Tuesday, March 20, 2018

MAJALIWA ATAKA SULUHISHO MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA


Na Mwandishi wetu,

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Mawaziri wa Afya kutoka nchi tisa za Afrika kutoa mapendekezo ya namna ya kutokomeza magonjwa yasiyo ambukiza, kwa wakuu wa nchi hizo ili yafanyiwe kazi haraka.

Aliyasema hayo jana Machi 19 mwaka huu wakati alipokuwa akifungua Mkutano wa 65 wa Mawaziri wa Afya, kutoka nchi tisa wanachama wa Jumuiya ya Afya kwa nchi za Afrika Mashariki, Kati  na Kusini (ECSA-HC).

Alisema kuwa magonjwa yasiyo ambukiza ni miongoni mwa magonjwa ambayo yameendelea kuwatesa wananchi kwa kiasi kikubwa, katika nchi nyingi za Bara la Afrika hivyo vyema mawaziri hao wakatoa mapendekezo ya namna ya kuyatokomeza.


Waziri Mkuu alifafanua kuwa magonjwa hayo, yanaweza kudhibitiwa kwa kuhamasisha wananchi kuboresha lishe na kusisitiza ulaji wa vyakula bora, kufanya mazoezi na kubadili mitindo ya maisha.

“Magonjwa yasiyoambukiza yanaongoza kwa kusababisha vifo katika baadhi ya nchi wanachama wa ECSA. Magonjwa haya yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya mfumo wetu wa lishe na maisha, hivyo ni muhimu suala hili likatafutiwa ufumbuzi”, alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu huyo alieleza kuwa magonjwa yasiyoambukiza pamoja na magonjwa mengine ya milipuko kama vile ebola, homa ya bonde la ufa, dengue, homa ya manjano yamekuwa kikwazo cha maendeleo kwa katika baadhi ya nchi.

Pia aliongeza kuwa sekta ya afya ni muhimu kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya nchi zote ikiwemo zilizoendelea na zinazoendelea, hivyo changamoto zote zinazoikabili zinapaswa kupewa kipaumbele katika utatuzi huo.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Jinsia, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema malengo ya mkutano huo ni kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazohusu sekta ya Afya na kuyapatia ufumbuzi.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Mawaziri wa Afya kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afya kwa nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini ambazo ni Tanzania, Malawi, Lesotho, Uganda, Kenya, Rwanda, Zambia, Zimbabwe na Muwakilishi kutoka nchini Mauritius.

Pia Katibu wa jumuiya hiyo Profesa Yoswa Dambisya, Muwakilishi wa Benki ya Dunia Dokta Paolo Belli pamoja na wadau wa sekta ya afya kutoka nchi hizo.

No comments: