Tuesday, March 20, 2018

WANAFUNZI 60 WA KIKE MBINGA WASHINDWA KUENDELEA NA MASOMO


Na Kassian Nyandindi,   
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa katika shule za Sekondari zilizopo Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, Wanafunzi 60 wa kike wanaosoma katika shule hizo wameshindwa kuendelea na masomo mwaka jana 2017 kutokana na kuwa na ujauzito.

Wazazi, walezi na jamii ndiyo wamenyoshewa kidole katika suala zima la malezi ya watoto wa kike, ambapo wamekuwa hawatoi ushirikiano wa kutosha hata pale mtoto huyo anapokuwa amepata ujauzito hususan Serikali inapotaka kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa wanaohusika na tatizo hilo.

Joseph Kapere ambaye ni Afisa elimu Sekondari wa Wilaya hiyo alisema hayo hivi karibuni, wakati alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha tathimini ya elimu kilichofanyika mjini hapa.


Kufuatia hali hiyo imeelezwa kuwa kwa kiasi kikubwa imekuwa ikichangia watoto hao kukatisha masomo yao.

Baadhi ya wadau wa elimu katika Wilaya hiyo, wamependekeza kuwa mwanaume yeyote atakayepatikana na kosa la kumpa mimba mwanafunzi, apewe adhabu ya kifungo cha maisha badala ya sheria ya sasa ya kifungo cha miaka 30.

Adelgot Milinga Afisa Mtendaji wa kata ya Litumbandyosi alisema kwamba iwapo Serikali itaongeza adhabu kwa watu hao itasaidia kupunguza tatizo hil kwa wanafunzi na watoto wadogo chini ya umri wa miaka 18 ambalo linao onekana kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Alieleza kuwa kifungo cha miaka 30 bado hakioneshi kama ni suluhisho la kuweza kumaliza tatizo la mimba kwa wanafunzi wa kike ndani ya Wilaya hiyo na hata katika Mikoa mingine hapa nchini hivyo Serikali iangalie namna kuongeza adhabu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye alisema hadi sasa ni asilimia 90 ya watoto ambao walioandikishwa kuanza elimu ya msingi Wilayani humo katika kipindi cha mwaka huu na wale waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza ndiyo wanaotakiwa kuripoti katika shule walizopangiwa.

Kutokana na tatizo hilo, ameagiza hadi kufikia tarehe 30 mwezi huu watoto wote waliopo majumbani ambao wazazi bado hawajawapeleka shule, wahakikishe wanakwenda shule kabla ya kuanza msako kabambe wa kufuatilia watoto na wazazi wao.

Nshenye alisema ni aibu kubwa kuona Wilaya hiyo imeshuka kitaaluma kwa kushika nafasi ya 137 katika matokeo ya darasa la saba mwaka 2017 kutoka nafasi ya 127 katika matokeo ya mwaka 2016.

Amewataka wadau wa elimu kutafuta majawabu ya kumaliza tatizo hilo mapema huku akiwaagiza Watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha kwamba wanashirikiana na vyombo vingine vya sheria vya Serikali kuwasaka watoto na wazazi wao.

No comments: