Tuesday, March 20, 2018

MAKILLAGI ATAKA UWT KUWA KIMBILIO LA WANAWAKE


Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

JUMUIYA ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) imesema kuwa wanataka kuona kwamba inakuwa kimbilio kubwa kwa Wanawake, katika kuanzisha vikundi vya ujasiriamali ambavyo vitaweza kuwakomboa waweze kuondokana na umaskini.

Vikundi hivyo imesisitizwa kuwa viundwe na kusajiliwa kisheria ili kuweza kukuza uchumi wa akina mama na kujenga mshikamano wa pamoja utakaowafanya waache tabia ya kuwa na makundi ambayo hapo baadaye yanawagawa wao na chama kwa ujumla.

Amina Makillagi ambaye ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) alisema hayo juzi, alipokuwa katika ziara yake ya siku mbili Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma akitembelea kujionea maendeleo ya umoja huo.


Alisema kuwa hizi ni zama za ukweli na uwazi ambapo viongozi umefika wakati sasa wa kusimamia maadili mema ya mwanachama ili waweze kuepukana na matendo yanayorudisha nyuma maendeleo yao.

Pia alisisitiza kuwa katika vikundi hivyo wanapaswa wajishughulishe na shughuli za ufugaji wa mifugo ya aina mbalimbali, kilimo na biashara ndogo ndogo ambavyo vitaweza kuwaingizia kipato na kusukuma mbele maisha yao.

No comments: