Tuesday, March 13, 2018

SERIKALI KUTUMIA TRILIONI 32.4 MWAKA WA FEDHA 2018/2019



Na Mwandishi wetu,
Dodoma. 

IMEELEZWA Serikali imepanga kukusanya na kutumia shilingi trilioni 32.476 kwa mwaka ujao wa fedha wa 2018/2019.
Dokta Philip Mpango.

Akiwasilisha mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na kiwango cha ukomo wa bajeti kwa mwaka 2018/2019, Waziri wa Fedha na Mipango, Dokta Philip Mpango alisema kuwa ukomo wa bajeti umezingatia upatikanaji wa mapato.

Dokta Mpango alisema katika mwaka huo Serikali imepanga kutumia shilingi trilioni 20.468 kwenye matumizi ya kawaida sawa na asilimia 63 ya bajeti yote.

Matumizi hayo alifafanua kuwa yanajumuisha shilingi trilioni 10 zitakazolipa deni la Taifa na shilingi trilioni 7.369 mishahara ya watumishi wakati shilingi trilioni 3.094 zikielekezwa kwenye matumizi mengine.

 
Dokta Mpango alisema Serikali itatumia shilingi trilioni 12 sawa na asilimia 37 kutekeleza miradi ya maendeleo.

Kiasi hicho, kinajumuisha shilingi trilioni 9.876 sawa na asilimia 82.3 kutoka vyanzo vya ndani na shilingi 2.13 sawa na asilimia 17.7 kutoka nje.

Jumla ya mapato ya ndani pamoja na makusanyo ya Halmashauri yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 20.894 ambayo ni sawa asilimia 64 ya bajeti yote.

“Kati ya mapato hayo yatokanayo na kodi yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 18 sawa na asilimia 13.6 ya Pato la Taifa”, alisema.

Alisema kuwa mapato yasiyokuwa ya kodi yanatarajiwa kufika shilingi trilioni 2.158 wakati vyanzo vya Halmashauri vikikusanya shilingi bilioni 735.6.

Dokta Mpango aliongeza kuwa vyanzo vingine vinavyotarajiwa kufanikisha utekelezaji wa bajeti hiyo ni misaada na mikopo yenye masharti nafuu kiasi cha shilingi trilioni 2.676 kutoka kwa washirika wa maendeleo ambazo ni sawa na asilimia nane ya bajeti hiyo.

Katika mwaka ujao, alieleza kuwa Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 5.793 kutoka soko la ndani ambazo kati ya hizo, shilingi trilioni 4.6 zitatumika kulipia hati fungani na dhamana za Serikali zinazoiva.

Shilingi trilioni 1.193 zinazozidi kwenye mikopo hiyo ya ndani ambazo ni sawa na asilimia 0.9 ya pato la Taifa, amesema ndilo deni jipya.

“Ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miundombinu, Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 3.111 kutoka soko la nje”, alisema Dokta Mpango.

No comments: