Friday, March 9, 2018

MLEMAVU WA MIGUU KICHANGANI TUNDURU APEWA MSAADA WA BAISKELI MAGURUDUMU MATATU

Mkurugenzi wa Kampuni ya D&G Export Company Limited, Geofrey Kalamba (kushoto) akikabidhi Baiskeli ya magurudumu matatu yenye thamani ya shilingi 320,000 kwa Fatma Kaluma ambaye ni Mlezi wa mwanafunzi Shaibu Mpoto aliyeketi kwenye Baiskeli hiyo, anayesoma darasa la saba shule ya Msingi Kichangani Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma.


Na Mwandishi wetu,      
Tunduru.

MWANAFUNZI wa darasa la saba, Shaibu Mpoto ambaye ni wa shule ya Msingi Kichangani kata ya kichangani Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, anashindwa kuendelea na masomo katika shule hiyo baada ya kuugua ugonjwa wa kupooza miguu kwa muda mrefu.

Tatizo hilo ambalo limempata mwanafunzi huyo ni miaka minne sasa imepita, lakini baada ya kupata msaada wa Baiskeli yenye magurudumu matatu hivi sasa inamsaidia kwenda shuleni kuhudhuria vipindi vya masomo na kurudi nyumbani kwake Kichangani ambako anaishi na ndugu zake.

Kampuni ya D&G Export Limited inayojishughulisha na kazi ya ununuzi wa mazao na utunzaji wa Korosho Tunduru na Liwale Mkoa wa Lindi, ndiyo ambayo imeweza kumpatia Baiskeli hiyo na kuondoa adha aliyokuwa akiipata kwa muda mrefu mwanafunzi huyo.


Shaibu alikata tamaa katika kutimiza ndoto yake ya kuendelea na masomo kikamilifu kutokana na kupata ugonjwa huo, ili hapo baadaye aweze hata kujitegemea mwenyewe na kutoa mchango wake kwa Taifa hili.

Akizungumza jana na Mwandishi wetu alisema kuwa alianza kupooza miguu yote miwili mwaka 2014 akiwa darasa la tatu, hivyo anashukuru kwa kuweza kupata msaada huo.

Wakati mwingine ndugu zake Shaibu walikuwa wakilazimika kumbeba mgongoni kumpeleka shule na kwamba baada ya kupata msaada huo imekuwa ni mkombozi mkubwa kwao.

“Nashukuru kwa msaada huu ambao utanisaidia kwenda shuleni na kurudi nyumbani, hata kwenda maeneo mengine bila kuhitaji kubebwa na mtu”, alisema Shaibu.

Vilevile mlezi wa Shaibu ambaye ni Bibi yake, Fatma Kaluma alisema kuwa hivi sasa ataweza kupata muda wa kupumzika kumbeba kila siku asubuhi na jioni, na kuweza kufanya kazi nyingine za kujiongezea kipato kutokana na hapo awali alishindwa kufanya hivyo kutokana na tatizo hilo la mjukuu wake.

Fatma anawaomba Wasamaria wema waendelee kumsaidia mjukuu wake, kwani hivi sasa anahitaji kupata sare za shule na vifaa vya masomo darasani kama vile daftari, kalamu za kuandikia na vitabu vya kusoma.

Mkurugenzi wa Kampuni hiyo iliyotoa msaada huo, Geofrey Kalamba alisema kuwa walikuwa wakiona huruma namna mwanafunzi huyo alivyokuwa akikaa nyumbani kwa muda mrefu na kupata mateso ya kushindwa kuhudhuria kikamilifu vipindi vya masomo darasani, hivyo waliona ni vyema sasa wampatie Baiskeli ambayo wameinunua kwa gharama ya shilingi 320,000 ili iweze kumsaidia katika maisha yake.

No comments: