Tuesday, March 20, 2018

DC ATAKA WATUMISHI WADANGANYIFU MADABA WASHUGHULIKIWE


Na Muhidin Amri,    
Madaba.

MKUU wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma, Pololet Mgema amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Shafi Mpenda kuwachukulia hatua za kinidhamu Watumishi wake waliopo katika Halmashauri hiyo ambao wamehusika na kufanya udanganyifu katika ujenzi wa vyumba vya madarasa shule ya msingi Kibulang’ombe iliyopo kata ya Likalangiro Wilayani hapa.

Udanganyifu huo umefanyika kwenye ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule hiyo na kusababisha ujenzi kusimama kwa muda kufuatia watu waliopewa dhamana ya kusimamia hilo kukiuka taratibu husika hasa katika manunuzi vifaa ikiwemo bati geji 32 badala ya geji 30 kama ilivyoagizwa na Serikali jambo ambalo Mkuu huyo wa Wilaya amesimamisha ujenzi huo kwa muda mpaka tatizo hilo litakapokwisha.

“Nimewatuma watu wangu kufuatilia kila mradi unaotekelezwa katika Halmashauri yako, walipofika pale shule ya msingi Kibulang’ombe kwa kweli  ni masikitiko makubwa kwani bati zilizonunuliwa ni geji 32 badala ya geji 30, kwa hiyo nakuagiza wewe na wataalamu wako lazima mfuatilie hili ili kujiridhisha ni nani aliyehusika kufanya udanganyifu”, alisema Mgema.


Katika kata ya Likalangiro alisema bado kuna miradi mingi haijakwisha ujenzi wake, hivyo ni lazima Viongozi husika wa Halmashauri wahakikishe wanatafuta fedha kwa ajili ya kuikamilisha ili wananchi waweze kuitumia kwa faida ya kizazi cha sasa na kile kijacho.

Mgema aliitaja miradi ambayo bado haijakamilika ni pamoja na madarasa, matundu ya vyoo na majengo ya maabara huku akisisitiza kuwa wakati umefika kwa uongozi wa Halmashauri ya Madaba kuona umuhimu wa kutenga pia fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi yote viporo kabla ya kuendelea na ujenzi wa miradi mipya.

Alisema kuwa katika ulimwengu wa sasa tunahitaji kuzalisha wasomi wa masomo ya Sayansi ambao watakaokuja hapo baadaye kufanya kazi katika viwanda vitavyoanzishwa sasa, badala ya kutafuta wataalamu wengine kutoka nje ya Wilaya hiyo na kuagiza kuanzia sasa kila shule iwe na jengo la masomo ya Sayansi (maabara) ambalo limekamilika na vifaa vyake vyote vya masomo darasani ambavyo vitasaidia wanafunzi waweze kusoma vizuri.

Bila kufanya hivyo aliongeza kuwa tutahitaji wasomi wengi kutoka nchi za nje kama vile Kenya na Uganda kwa ajili ya kuja kufanya kazi hapa Tanzania katika viwanda vyetu, na kwamba ni lazima sasa katika Halmashauri hiyo kuhakikisha wanazalisha wasomi wa masaomo ya Sayansi watakaokuwa msaada katika viwanda vyetu vya hapa nchini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Vastus Mfikwa alikiri uwepo wa miradi kiporo katika maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya yake, ambapo alihaidi kuwa katika bajeti ya mwaka 2018/2019 kipaumbele kilichopo ni kukamilisha miradi yote ambayo ujenzi na uwekaji wa vifaa husika ndani yake haujakamilika.

No comments: