Thursday, March 22, 2018

MCHINA KUENDELEA NA UKARABATI BARABARA MANISPAA SONGEA

Moja kati ya barabara za Manispaa ya Songea ya FFU Matogoro ambayo inafanyiwa ukarabati.
Na Albano Midelo,      
Songea.

HATIMAYE Kampuni ya kimataifa ya Serikali ya China, inayoitwa China Sichuan International Co-operation, kufikia Machi 25 mwaka huu itaanza rasmi ukarabati wa barabara za Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, kwa kiwango cha lami nzito.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Mkoani humo, Mhandisi Samwel Sanya alisema hayo leo kuwa Kampuni hiyo tayari imesaini mkataba baina yake na Halmashauri ya Manispaa hiyo.

Alifafanua kuwa mkataba unaonesha kuwa, ukarabati wa barabara hizo zenye urefu wa kilometa 10.3 utaanza Machi 25 mwaka huu na unatarajia kukamilika Septemba 30 mwaka 2019.


“Mkataba ni wa miezi 18, fedha ambazo zinatumika katika ukarabati huo ni bilioni 10.96, Mkandarasi wa sasa anaongeza kilometa zaidi ya mbili, pia ataweka taa za barabarani”, alisema Sanya.

Halmashauri ya Manispaa ya Songea ilivunja Mkataba wa ujenzi wa lami nzito yenye urefu wa kilometa 8.6 kati yake na Kampuni ya Lukolo yenye makao makuu yake jijini Dar es salaam, baada ya Kampuni hiyo kukiuka masharti ya mkataba wa miaka miwili uliomalizika Juni 30 mwaka 2017.

Baada ya muda huo kumalizika Mkandarasi huyo aliingizwa kwenye tozo (Liquidated Damage) kwa siku 100 ambapo Oktoba 8 mwaka jana ndiyo siku 100 alizopewa Mkandarasi huyo zilimalizika hivyo Manispaa ilivunja mkataba rasmi na Kampuni hiyo ya Lukolo.

Pia kuvunjwa kwa mkataba huo, Manispaa ya Songea ilianza mchakato wa kumtafuta Mkandarasi mwingine ambapo amepatikana Mkandarasi wa Kampuni ya China Sichuan International, ambaye ataendeleza kazi ya ukarabati barabara na kwamba Manispaa haijapata hasara yeyote baada ya kuvunjwa kwa mkataba wa Mkandarasi wa kwanza.

Fedha za mradi huo ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 14 zimetolewa na Benki ya Dunia chini ya Mpango wa kuzijengea uwezo Serikali za mitaa (ULGSP) mpango huo, unakusudia kuendeleza miundombinu ya Halmashauri za miji na Manispaa 18 za Tanzania Bara ikiwemo Manispaa ya Songea.

Mradi huo ambao ulianza Juni Mosi 2015 ulitarajiwa kukamilika Juni 30 mwaka 2017 na kwamba Barabara za Manispaa hiyo ambazo zipo kwenye mradi huu ni FFU hadi Matogoro yenye urefu wa kilometa 3.2, barabara ya Songea Girl’s hadi Mateka yenye urefu wa kilometa 1.5 na barabara ya Mwembechai hadi Bombambili yenye urefu wa kilometa 2.6.

Barabara nyingine ni Mitumbani hadi Yapenda yenye urefu wa kilometa moja, barabara ya Polisi hadi Stendi ya Mlilayoyo yenye urefu wa kilometa 0.45.

No comments: