Sunday, March 25, 2018

MANISPAA SONGEA YAINGIA MKATABA UJENZI WA STENDI MPYA YA KISASA

Hili ni eneo la kata ya Tanga ambalo ujenzi wa Stendi ya kisasa katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma unatarajiwa kuanza kujengwa.

Na Kassian Nyandindi,         
Songea.

KAMPUNI ya Serikali ya China, inayoitwa China Sichuan International Cooperation imesaini mkataba wa miezi 18 na Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, kwa ajili ya ujenzi wa Stendi mpya ya mabasi katika eneo la Tanga kuanzia Aprili Mosi mwaka huu.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo, Mhandisi Samwel Sanya alisema kuwa Mkataba huo unaanzia Machi 25 hadi Septemba 30 mwaka 2019.

Alisema kuwa zaidi ya Shilingi Bilioni sita zitatumika katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa stendi hiyo ya kisasa na kwamba lengo la kufanya hivyo ni kuendana na kasi ya ukuaji wa mji, hivyo Manispaa iliamua kutenga eneo la kituo kikuu cha mabasi kuwa katika mtaa huo wa Tanga ikiwa ni umbali wa takribani kilometa 14 toka mjini Songea.


“Fedha za mradi huu wa stendi zimetolewa kupitia Benki ya dunia, jumla ya hekari 29 zimetwaliwa katika eneo hilo ili kupitisha stendi ambapo hekari 20 zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 32 tayari zimelipwa kama fidia kwa wananchi”, alisema Sanya.

Kampuni ya China Sichuan International Cooperation imesaini pia mkataba wa miezi 18 wa ukarabati wa barabara ya lami nzito katika Manispaa hiyo yenye urefu wa kilometa 10.3 kwa thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni kumi.

Fedha za miradi hiyo ya barabara na stendi zimetolewa na Benki ya dunia chini ya Mpango wa kuzijengea uwezo Serikali za Mitaa (ULGSP), mpango huo unakusudia kuendeleza miundombinu ya Halmashauri za miji na Manispaa 18 za Tanzania bara ikiwemo hiyo ya Songea.

No comments: