Saturday, March 10, 2018

JAJI MKUU ATAKA NAKALA ZA HUKUMU ZITOLEWE KWA WAKATI



Profesa Ibrahimu Juma.
Na Ferdinand Shayo,    
Arusha.

JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma ameonesha kutoridhishwa kwake na mfumo wa utoaji wa taarifa mbalimabli za Kimahakama ikiwa ni pamoja na matamshi ya lugha, urasimu unaofanywa na baadhi ya Watumishi wa Mahakama katika utoaji wa nakala za hukumu.

Profesa Juma ametoa kauli hiyo leo jijini Arusha katika ufunguzi wa kikao kazi cha watendaji na wataalamu wa Mahakama, kwa lengo la kutathimini utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka mitano na utekelezaji wa mradi wa maboresho wa utoaji wa huduma za Mahakama hapa nchini.

Katika kikao hicho Jaji Mkuu, alitolea mfano andiko la benki ya dunia linalozungumzia ukosefu wa taarifa kwa umma kuhusu mashauri na kasi ndogo ya kuchapishwa kwa nakala za hukumu, huku nakala hizo zikichapishwa kwa lugha ya kiingereza na wakati mwingine kisheria zaidi.


Vilevile katika kuitathimini taarifa ya benki ya dunia kuhusu utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania, alisema meagiza kila Mahakama kuwa na miongozo kwa watumiaji wa chombo hicho ili kuwasaidia wakati wa utafutaji wa huduma mbalimbali za kimahakama.

Mpango unaojadiliwa na watendaji hao wa ngazi mbalimbali za kimahakama ni ule wa miaka mitano kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2019/2020 unaofadhiliwa na benki ya dunia ukilenga maboresho ya utoaji wa huduma za kimahakama hapa nchini.

No comments: