 |
Waziri Bernad Membe akipokelewa jana na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, wakati alipowasili katika Ofisi za makao makuu ya CCM mkoani humo zilizopo katika Manispaa ya Songea. |
 |
Upande wa kushoto, Waziri Bernad Membe akikabidhiwa fomu ya watu ambao wamemdhamini mkoani Ruvuma katika harakati zake za kutaka kugombea Urais. Anayemkabidhi fomu hiyo ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo, Oddo Mwisho. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WAZIRI wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa,
Bernad Membe amesema iwapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitampa ridhaa ya kugombea
nafasi ya Urais na kushinda katika uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba
mwaka huu jambo la kwanza atakalolifanya kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma, ni
kujenga viwanda vingi vitakavyosaidia kusindika vyakula kwa ajili ya kuongeza
thamani ya mazao yanayolimwa mkoani humo, ili wakulima wake waweze kukua
kiuchumi.
Hayo yalisemwa jana na Waziri Membe alipokuwa akizungumza na baadhi
ya wanachama wa CCM, alipokuwa katika harakati zake za kutafuta wadhamini ndani
ya chama hicho mkoani hapa, ambapo zaidi ya wanachama 5600 walijitokeza
kumdhamini mgombea huyo wa Urais.
“Namuomba sana Mungu endapo chama changu kitanipa ridhaa ya
kupeperusha bendera na hatimaye kushinda nafasi hii mwezi Oktoba, basi jambo la
kwanza nitakalowafanyia ndugu zangu wanaruvuma ni kujenga viwanda ili vyakula
vinavyolimwa hapa kwetu, viweze kusindikwa katika ubora unaokubalika”, alisema Waziri
Membe.
Aidha amewataka wanachama wa chama hicho kutowaogopa wagombea
wengine, ambao wameonesha dhamira ya kugombea urais kupitia tiketi ya CCM.
Waziri Membe alisema wanachopaswa ni kuwauliza maswali juu ya
uadilifu na uwajibikaji wao, kwa wananchi hatua itakayowawezesha kutambua nani
anafaa kusimamishwa na kugombea katika kinyang’anyiro hicho.