Sunday, December 20, 2015

AMCHARANGA MKEWE MAPANGA NA KUTOKOMEA KUSIKOJULIKANA



Na Steven Augustino,

Tunduru.

BINTI mwenye umri wa miaka 18 aliyetambuliwa kwa jina la, Stawa Waziri amelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Tunduru mkoa wa Ruvuma akiwa hajitambui, baada ya kukatwa katwa mapanga na mumewe katika tukio lililohusishwa na wivu wa kimapenzi.

Aidha baada ya tukio hilo mumewe aliyemsababisha majeraha mwilini mwake, Rashid Mohamed (22) alikimbia na kutokomea kusikojulikana jambo ambalo liliwafanya majirani kuokoa maisha ya majeruhi huyo, kwa kumkimbiza kituo cha afya Nakapanya kwa ajili ya kumpatia huduma ya kwanza na baadaye alipelekwa katika Hospitali hiyo ya wilaya, kwa matibabu zaidi.

Taarifa za tukio hilo zimeripotiwa kuwa, lilitokea usiku wa kuamkia Disemba 19 mwaka huu kitongoji cha Mchololo kijiji cha Tulieni, katika kata ya Nakapanya wilayani Tunduru.


Mashuhuda wa tukio hilo walisema kwamba, kabla ya tukio hilo kutokea wanandoa hao walikuwa wakigombana kama ilivyo kawaida yao ambapo  mara kadhaa ugomvi wao, umekuwa ukitokea kutokana na mwanaume kutoamini nyendo za mkewe.

Diwani wa kata ya Nakapanya, Kubodola Ambali alisema katika tukio hilo Rashid alimjeruhi mkewe kwa kumkata sehemu mbalimbali za mwili wake na kumtelekeza ndani ya nyumba yao waliyokuwa wakiishi, kisha kutokomea kusikojulikana.

Akizungumzia tukio hilo Kaimu mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya hiyo, Dokta Mmari Zabroni pamoja na kukiri kuwepo kwa majeruhi huyo alisema majeruhi, bado anahitaji kuwa chini ya uangalizi wa maafisa tabibu kwa kipindi kirefu kutokana na hali yake kiafya kutokuwa nzuri.

Vilevile katika tukio hilo majeruhi huyo, ameumia vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo maeneo ya kichwa, usoni pamoja na mkono wa kulia.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba Polisi wamejipanga kumsaka mtuhumiwa huyo, ili aweze kupatikana na sheria ichukue mkondo wake.

No comments: