Thursday, December 24, 2015

MAJAMBAZI YAPORA MILIONI 2.7 MKOWELA TUNDURU



Na Steven Augustino,
Tunduru.

ZUHURA Ngaharo ambaye anaishi katika kijiji cha Mkowela wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, amevamiwa nyumbani kwake na watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi na kumpora fedha shilingi milioni 2.7 za mauzo ya duka lake.

Tukio hilo lilitokea majira ya usiku, Disemba 21 mwaka huu baada ya majambazi hao kumteka na kumlazimisha kuwapatia fedha hizo za mauzo.

Diwani wa kata ya Nakapanya, Kubodola Ambali alisema kuwa katika tukio hilo mama huyo ambaye ni mjane alivamiwa na watu wawili huku wakiwa na silaha ya moto, bunduki  na za jadi ambazo ni visu na mapanga jambo ambalo lilimtisha maisha yake.


Alisema baada ya kumteka, watu hao walimwamuru kuingia dukani na kuwapatia fedha hizo na asingefanya hivyo walikuwa wakimtishia kwamba wangepoteza maisha yake, yeye na watoto ambao anaishi nao nyumbani hapo.

Baada ya maharamia hao kupata kiasi hicho cha fedha, waliondoka na kutokomea kusikojulikana.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kuongeza kuwa tayari amekwisha tuma kikosi cha askari shupavu, kwa ajili ya kuwasaka watuhumiwa hao.

Aidha amewaomba wananchi, ambao wanaweza kuwa na taarifa zozote juu ya watu ambao wamekuwa wakifanya uhalifu katika matukio tofauti mkoani humo, kuwataja ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Endapo wataendelea kuwaficha watu hao, ipo hatari ya kuendelea kupata madahara makubwa yatakayosababishwa na wahalifu hao wanaowaficha, nawataka wananchi waendelee kujenga ushirikiano kwa kuwataja popote pale walipo ili tuweze kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya kisheria”, alisema.

No comments: