Sunday, December 13, 2015

MANISPAA YA SONGEA YAMPATA MEYA MADIWANI WATAKIWA KUWATUMIKIA WANANCHI

Mwandishi wa habari mkongwe hapa nchini, Cresensia Kapinga kushoto akila kiapo cha uaminifu  na madiwani wenzake wakati wa baraza la madiwani wa manispaa ya Songea mkoani Ruvuma. Kapinga aligombea udiwani katika kata ya Ndilimalitembo na kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Na Julius Konala,
Songea.

MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamefanya uchaguzi na kumpata mstahiki Meya mpya, Alhaj Mshaweji Abdul Hassan atakayeiongoza Manispaa hiyo kwa kipindi cha miaka mitano.

Uchaguzi huo ulifanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa hiyo, chini ya Mwenyekiti wake wa muda, Juma Ally ambaye ni Katibu tawala wa wilaya ya Songea na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wabunge, viongozi wa vyama vya siasa, serikali, madiwani na wananchi kutoka kata zote za Manispaa ya Songea.

Baada ya uchaguzi huo kufanyika Mwenyekiti huyo wa muda, alimtangaza Alhaj Mshaweji Abdul Hassan wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mstahiki meya wa Manispaa hiyo baada ya kushinda kwa kura 26 kati ya 30, dhidi ya mpinzani wake kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mussa Ndomba ambaye alipata kura 4.


Aidha katika uchaguzi huo, alimtangaza Consolata Kilowoko kupitia tiketi ya CCM kuwa mshindi nafasi ya Naibu meya kwa kupata kura 25 kati ya 30 huku mgombea wa CHADEMA, Martin Mlata akiwa amepata kura 5.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa baraza jipya la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea, aliwataka madiwani na watumishi wa Manispaa hiyo kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano kwa kufanya kazi ya kusimamia mapato na matumizi ya Halmashauri hiyo kwa weledi, uaminifu na uadilifu mkubwa.

Mwambungu ameonya pia madiwani na watumishi wazembe ambao wanafanya vitendo vya ubadhirifu na rushwa, kwa madai kuwa vinasababisha miradi mingi ya maendeleo ya wananchi kujengwa chini ya kiwango na kuisababishia serikali hasara, ambapo alisema serikali haitamfumbia macho mtu yeyote atakayebainika kutenda kosa hilo.

Awali akizungumza katika kikao hicho mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Alhaj Mshaweji Abdul Hassan aliwashukuru madiwani kwa kumchagua kwa kura nyingi, kuwa kiongozi wao huku akiwataka kumpa ushirikiano katika kulisukuma gurudumu la maendeleo ya Manispaa hiyo, bila ya kujali itikadi ya vyama vya siasa.

No comments: