Thursday, December 24, 2015

MUUGUZI AKAMATWA AKIUZA DAWA ZA SERIKALI


Na Muhidin Amri,

Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, linamshikilia Muuguzi msaidizi wa Zahanati ya kijiji cha Utwango wilaya ya Namtumbo mkoani humo, Agnera Luena kwa tuhuma ya kuuza dawa za serikali katika duka la mtu binafsi kinyume cha sheria.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Revocatus Malimi alisema tukio hilo lilitokea Disemba 23 mwaka huu majira ya saa nne asubuhi ambapo mtuhumiwa huyo akiwa kazini, aliiba dawa hizo na kwenda kuuza katika duka la Esha Tendwa lililopo katika kijiji cha Lusenti wilayani humo.

Revocatus Malimi.
Alisema mara baada ya kumkamata, Polisi walifanya upekuzi katika duka ambalo dawa hizo ziliuzwa na kukamata aina mbalimbali ambazo ziliibwa na mtuhumiwa huyo.

Kamanda Malimi alizitaja dawa zilizokutwa katika duka hilo ni, Paediatric cough Syrup chupa 13, Doxycline capsules kopo moja, Cotrimazole Syrup mbili, Diazepam Tables kopo moja, PPF injection moja na Amoxiline Oral Suspension mbili.

Aidha alizitaja dawa nyingine kuwa ni, Aspi -m- Chlorphenamine tablets moja, Alu 1x6 Packet 4, Alu 3x6 Packet 4, ambazo thamani yake bado haijajulikana.


Kamanda Malimi alifafanua kuwa mmiliki wa duka hilo, pia anashikiliwa kwa tuhuma hizo na muda wowote upelelezi utakapokamilka watafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi mkoani Ruvuma, kuendelea kutoa ushirikiano kwa kuwafichua wafanyakazi wa hospitali ambao wanajihusisha na vitendo hivyo viovu, kinyume na taratibu za kazi zao ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria na iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

No comments: