Monday, December 7, 2015

ANGUKO LA BENEDICT NGWENYA HILI HAPA AWASHANGAZA WENZAKE BAADA YA KUTOKOMEA KUSIKOJULIKANA


Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mgombea mmoja wa nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, ambaye pia ni Katibu wa siasa na uenezi mkoani humo, Benedict Ngwenya amewaacha hoi wanachama wenzake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbinga mkoani humo, baada ya kutokomea kusikojulikana ikiwa ni lengo la kukwepa aibu na kusikiliza matokeo ya nafasi hiyo aliyogombea.

Mwandishi wa habari hizi ambaye alishuhudia tukio hilo, katika Ofisi za CCM wilaya zilizopo mjini hapa, Ngwenya licha ya kuombwa na wanachama wenzake asiondoke katika eneo hilo hakuweza kuvumilia badala yake alipomaliza kupiga kura, aliingia kwenye gari gari lake na kuondoka.

Wakihojiwa na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti juu ya hali hiyo, Madiwani wenzake wa Chama hicho walisema kukimbia huko anakwepa aibu ya matokeo ya nafasi hiyo aliyogombea, ambayo awali alikuwa akitamba mtaani na kujipa nafasi kubwa ya ushindi.

Benedict Ngwenya.
“Sisi tumemshangaa sana, sote tuliambiwa hapa tusiondoke mpaka taratibu za uchaguzi zikamilike, lakini mwenzetu alipomaliza tu kupiga kura tulimuona akiaga ghafla na kuondoka huku akisema anasumbuliwa na tumbo”, walisema.

Ngwenya ambaye pia ni Diwani wa kata ya Mpepai katika Halmashauri ya mji huo, alipotafutwa kwa njia ya simu na mwandishi wetu, ili aweze kuthibitisha hilo ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa. 

Madiwani hao wa wilaya ya Mbinga kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, leo wamefanya uchaguzi wao ndani ya chama hicho na kuwateua wenyeviti watakaoweza kuongoza  Halmashauri zao, kwa kipindi cha miaka mitano.

Uchaguzi huo umeendeshwa kwa amani na utulivu, tofauti na chaguzi nyingine zilizopita ambapo kulikuwa na vurugu za hapa na pale huku ikifikia hatua baadhi ya wafuasi wa chama hicho, kuchoma moto Ofisi ya Katibu wa CCM wilaya.


Katibu wa Uchumi na fedha mkoa wa Ruvuma, Slim Mohamed ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo ametangaza matokeo majira ya mchana katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi, uliopo mjini hapa ambako chaguzi hizo zilikuwa zikiendeshwa.
Uchaguzi huo ulikuwa ukifanyika kwa Halmashauri ya mji wa Mbinga na ile ya wilaya ya Mbinga vijijini.

Kwa upande wa Halmashauri ya mji wa Mbinga, nafasi ya Mwenyekiti na idadi ya kura walizopata katika mabano, imechukuliwa na Ndunguru Kipwele ambaye ni Diwani wa kata ya Myangayanga aliyepata kura (15) na Makamu wake ikichukuliwa na Tasilo Ndunguru, Diwani wa kata ya Kikolo kwa kura (17).

Kipwele katika nafasi hiyo aliweza kuwa bwaga chini Katibu wa siasa na uenezi mkoa wa Ruvuma, Benedict Ngwenya ambaye pia ni Diwani wa kata ya Mpepai aliyepata kura (7) na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbinga ambaye ni Diwani wa kata ya Kagugu, Christantus Mbunda (1).

Pamoja na mambo mengine, Tasilo naye aliweza kuwa garagaza chini wapinzani wake ambao ni Aurelia Ntani kata ya Mbinga mjini ‘A’ aliyepata kura (2) na wa viti maalum tarafa ya Mbinga mjini, Imelda Mapunda kwa kura (3).

Vilevile kwa upande wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga vijijini, Mtarazaki Nchimbi kutoka kata ya Amani Makolo aliibuka mshindi kwa nafasi ya Mwenyekiti akipata kura (22) akifuatiwa na Makamu wake, Benard Komba kutoka kata ya Matiri aliyeweza kupata kura (22).

Mtarazaki alikuwa akipambana na wapinzani wake wawili, ambao ni Winfrid Kapinga ambaye alijitoa dakika za mwisho katika kinyang’anyiro hicho na Isaack Ndunguru aliyepata kura (16) huku Komba naye akiwaangusha chini Diwani wa kata ya Kigonsera, Zena Mijinga (5) na Joackimu Kowelo kutoka kata ya Mikalanga aliyeambulia kura (11).

Hata hivyo baada ya chaguzi hizo ndani ya chama kufanyika na kuwapata Wenyeviti hao wateule, ratiba kamili ya kuwapeleka katika vikao vya baraza la Madiwani na kufanyika uchaguzi wa kuwathibitisha kuwa wenyeviti kamili, itatolewa wakati wowote kuanzia sasa.


  

No comments: