Wednesday, December 9, 2015

MBINGA VIJIJINI WASHIRIKI KIKAMILIFU KUFANYA USAFI MWAMENGO AAGIZA UJENZI WA VYOO BORA


Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

MKURUGENZI Mtendaji Halmashauri wilaya ya Mbinga vijijini mkoani Ruvuma, Venance Mwamengo amewaagiza watendaji wa vijiji na kata wilayani humo kutoa elimu kwa wananchi juu ya ujenzi wa vyoo bora vya kisasa, ili waweze kuepukana na magonjwa mbalimbali ya mlipuko.

Agizo hilo lilitolewa na  Mkurugenzi huyo, baada ya kubaini ujenzi wa vyoo hivyo katika wilaya hiyo maeneo ya vijijini umekuwa ni wa kiwango cha chini, ambao hauzingatii usafi wa mazingira kwa afya ya binadamu.

Rais wa Tanzania, John Magufuli.
“Naagiza kuanzia sasa, watendaji wote ndani ya wilaya hii elimisheni wananchi wajenge vyoo bora vya kisasa, hili suala la usafi sio hiari nataka watu walitekeleze kwa vitendo ili tulinde afya zetu”, alisema Mwamengo.

Mwamengo alitoa rai hiyo leo, alipokuwa katika kata mbalimbali wilayani humo kwenye zoezi la kushiriki na kuhamasisha watu kufanya usafi ambalo linaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru wa Tanzania bara hapa nchini.

Alipokuwa katika kata ya Maguu, Mkurugenzi huyo aliweza pia kutoa onyo kali kwa mfanyabiashara Steven Haulle ambaye anauza bidhaa mbalimbali katika jengo moja lililopo karibu na soko la kata hiyo, ambapo alimpatia siku saba ahakikishe anakarabati choo chake ambacho mfumo wa maji taka na shimo lake la kuhifadhia taka hizo, lilikuwa limebomoka huku likitoa harufu jambo ambalo ni hatari kwa afya ya mtumiaji na watu wengine, wanaozunguka katika eneo hilo.


Wakati anatoa onyo hilo, aliutaka uongozi wa kata hiyo kumpatia taarifa kamili ya utekelezaji wa agizo hilo na endapo mfanyabiashara huyo hatatekeleza achukuliwe hatua za kisheria, ikiwemo kulipa faini ya shilingi 50,000 au kufikishwa Mahakamani.

“Ndugu yangu usipotimiza hili, funga shughuli za biashara yako kabla hatujachukua hatua nyingine mbele, nasisitiza kwenu viongozi wa kata zoezi hili ni endelevu hamasisheni wananchi wafanye usafi kuanzia majumbani kwao, ikiwemo na ujenzi wa vyoo bora”, alisema.

Zoezi hilo la kuhamasisha wananchi kutekeleza suala la usafi hapa katika wilaya ya Mbinga vijijini, lilianza mapema Desemba Mosi mwaka huu ambapo mwandishi wetu ameshuhudia wananchi katika maeneo mbalimbali wilayani humo wakihamasika kuzoa taka ngumu, kuchimba mashimo ya kuhifadhia taka hizo na baadaye huziteketeza kwa kuchoma moto.

Katika kata ya Mapera, akina mama na wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kata hiyo nao walikuwa wamevalia sare za chama hicho huku wakijigawa katika makundi na kushiriki kufanya usafi katika maeneo ya shuleni, kituo cha afya Mapera na majumbani kwao.

Vilevile kijiji cha Nyoni wilayani humo, mwandishi wa habari hizi alishuhudia Mwenyekiti wa kijiji hicho, Aghaton Lupogo akiwa anaongoza kundi la watu wakifanya usafi kwa pamoja katika eneo wanalofanyia mnada kijijini hapo ambalo lilikuwa limeshamiri uchafu wa taka ngumu, ambapo walikuwa wakizikusanya na kuziteketeza kwa moto.

Hata hivyo Lupogo alipohojiwa alisema kwamba, agizo la Rais John Magufuli “Hapa kazi tu” wamelipokea kwa mikono miwili na hivyo hawanabudi kulifanyia utekelezaji, kama vile kuzingatia suala la usafi ili waweze kuepukana na magonjwa mbalimbali.

No comments: