Thursday, December 24, 2015

MKURUGENZI TUNDURU ASHAURI HALMASHAURI YAKE ISHTAKIWE BARAZA LA ARDHI



Na Steven Augustino,
Tunduru.

BAADHI ya wananchi wa kijiji cha Nakayaya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wamegoma kupokea fidia zao walizotakiwa kulipwa na Halmashauri ya wilaya hiyo, ikiwa ni malipo ya fidia ya ardhi na mashamba yakiwemo na majumba wanayoishi ambayo yalipimwa na kuwataka wahame.

Mgomo huo wameufanya takribani miaka mitatu sasa, ambapo maeneo hayo yalipimwa kwa lengo la kuweka makazi kwa mfumo wa ramani ya mipango miji ya wilaya hiyo.

Kufuatia hali hiyo wananchi hao, wamemuomba Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi,  William Lukuvi kuingilia kati na kuwasaidia kupata haki zao za msingi zinazoonekana kutaka kuporwa na viongozi hao wa Halmashauri, wanaotumia mbinu za ujanja ili kutaka kupora haki za wananchi hao kwa lengo la kujinufaisha wenyewe baada ya kupima, kuyagawa kwa watu wengine na kuwatimua katika maeneo yao.


Wananachi hao walisema wamelazimika kupeleka maombi hayo kwa Waziri Lukuvi, kutokana na wao kuwa na matumaini ya utendaji wake na kwamba endapo atachelewa kuchukua hatua, ipo hatari ya kuzuka kwa mapigano kati yao na watu waliouziwa maeneo hayo na halmashauri hiyo, kwani hivi sasa wamekuwa wakifanya uhalifu mkubwa wa kukata mazao yao ya kudumu waliyopanda ikiwemo miti ya matunda, iliyopo katika maeneo hayo.

Wakifafanua juu ya hali hiyo kwa nyakati tofauti, walisema kilichowasukuma kuchukua maamuzi hayo   kinatokana na kubaini uwepo wa mchezo mchafu ulioambatana na vitendo vya uchakachuaji wa haki zao, uliopangwa kutekelezwa na viongozi wa Halmashauri yao.

Mmoja kati ya wasemaji wa wahanga hao, Jafary Muhyela alisema kuwa miongoni mwa vitu vilivyowafanya wasipokee cheki za malipo yao, ni kitendo cha usiri uliowekwa katika utaratibu wa malipo hayo ambayo hayaelezi uwazi na taratibu zilizotumika juu ya viwango halisi vya malipo.

Alisema hundi hizo ambazo ziliandikwa mwezi wa nne mwaka 2013, pamoja na kuonesha majina ya walengwa wa malipo hayo lakini hundi hazikuonesha kiasi cha fedha walizostahili kupokea na badala yake, walitakiwa kupokea hundi hizo zikiwa ndani ya bahasha zimefungwa huku kukiwa na maelekezo ya kuwataka wakazifungulie benki, wakiwa hawajui kiasi halisi cha fedha walichopokea.

Wananchi wengine waliogoma kupokea hundi hizo ni Longinus Rihard, Fatuma Mlanda, Laika Hamis, Daud Gwasa na Rashid Gwasa.

Kadhalika wengine ni Zainabu Gwasa, Rihard Ngonyani, Cosmas Mwimba, Mohamed Gwasa, Rukia Isaa, Magreth Mhyela na Jafary Muhyela ambaye alitakiwa kupokea miongoni mwa hundi hizo na kwamba hata wakati tathimini ya fidia zao ilipofanyika, wao hawakupatiwa hata nakala ya kumbukumbu za mali zao.

Alisema wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo hawakushirikishwa kikamilifu,  jambo ambalo ni ukiukwaji wa sheria ya ulipaji wa fidia ya ardhi inayoelekeza kwamba baada ya kufanyika kwa tathimini, wahusika walipwe ndani ya miezi sita.

Jambo jingine lililowashangaza ni  kitendo cha viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru, kuwanyima wamiliki wa mashamba hayo hata kipande cha kujenga katika ardhi wanayoimiliki kimila kwa muda mrefu, ambapo taarifa zinaeleza kuwa wazee hao walikimbilia katika maeneo hayo wakati wa vita vya Majimaji jambo wanalolitafsiri kuwa kitendo hicho ni ukiukwaji wa taratibu za haki za binadamu.

Walipotakiwa kuzungumzia mkanganyiko huo, Ofisa ardhi na maliasli wa  wilaya hiyo, Japhet Mnyagala na wa mipango miji mji wa Tunduru, Naon Chalale walikataa kuzungumzia juu ya malalamiko hayo wakisema kwamba wao siyo wasemaji juu ya suala hilo.

Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Tina Sekambo alikiri kuwepo kwa mgogoro huo na kuongeza kuwa kilichofanywa na uongozi huo ni halali, kwani taratibu haziruhusu kuwekwa wazi siri za mtu yeyote.

"Kilichofanywa na wataalamu wangu  kipo sahihi, kwani taratibu na miongozo ya ulipaji wa fedha haziruhusu kuwekwa wazi kwa kila mtu”, alisema Sekambo na kuongeza kuwa kutokana na kusuasua kwao kupokea malipo hayo tayari cheki zao zimekwisha muda wake (zimechacha) Oktoba 27/2013.

Sekambo aliendelea kufafanua kuwa wananchi hao wangepokea malipo hayo na baada ya kutafakari juu ya mapunjo wanayozungumzia, wangeandika barua za malalamiko ya kuomba kuongezewa malipo.

Alisema kwa sasa Halmashauri yake haijui itawasaidiaje na akawashauri kwenda kuishitaki katika baraza la ardhi, ili waweze kufikia muafaka juu ya mgogoro huo.

No comments: