Thursday, December 24, 2015

NGAGA AWATAKA WANAMBINGA KUPANDA MITI KWA WINGI



Na Muhidin Amri,
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga amewataka wananchi wa wilaya hiyo kutumia mvua zinazoendelea kunyesha  katika msimu wa mwaka huu, kwa kupanda miti  kwa wingi  ili kujiongezea kipato baada ya kuonekana zao hilo ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya kukuza mapato na uchumi, kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Senyi Ngaga.
 
Aidha aliwataka waache tabia ya kukata miti hovyo na kuchoma moto misitu hasa nyakati za kiangazi kipindi wanapoandaa mashamba yao, kwa ajili ya shughuli za kilimo huku akiongeza kuwa tabia hiyo imekuwa ikisababisha uharibifu wa mazingira na  virutubisho vya  udongo hupotea.
 
Ngaga alitoa wito huo  mwishoni mwa wiki, alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Amani Makolo wakati walipokuwa katika kazi ya upandaji miti, kata ya Amani Makolo wilayani humo.

 
Alisema kuwa changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira, imejitokeza katika maeneo yanayozalishwa kwa wingi zao la mahindi na kwenye misitu ya asili, kasi ya ukataji miti na uchomaji moto ni kubwa.

 Kadhalika aliwaagiza maofisa tarafa, kushirikiana na watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha wanawachukulia hatua wale wote wenye tabia ya kukata na kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji kwenye maeneo ya vyanzo vya maji, na endapo wataachwa bila kuwachukulia hatua huenda likatokea tatizo kubwa la upotevu wa vyanzo hivyo.

“Niwaombe wananchi waache kulima kwenye vilele vya milima na vyanzo vya maji, kumbukeni maji ni uhai na tegemeo kwa viumbe vyote hai na vile visivyo hai hivyo naagiza kila kijiji kihakikishe kinafuata taratibu na sheria ndogo zitakazosaidia kuwabana wale wote wanaojihusisha na uharibifu wa mazingira”, alisisitiza.

Awali katika taarifa yake Ofisa misitu wa wilaya hiyo, Vicent Mwafute alisema kuwa lengo la wilaya hiyo ni kukuza miche milioni 3,500,000 kila mwaka na kwamba  kuanzia mwaka 2010 mpaka kufikia mwezi Disemba mwaka jana, jumla ya miche milioni 11,386,648 imekuzwa na kupandwa kwa hekta 6,325 sawa na asilimia 90 ya upandaji.

Mwafute alisema changamoto zinazoikabili wilaya ya Mbinga, katika kutekeleza mpango huo wa kupanda miti kila mwaka ni pamoja na elimu ya uhifadhi wa mazingira, upandaji miti na kuitunza kama mazao mengine ambapo bado wananchi hawajaipokea kikamilifu na kwamba ili kufanikisha hilo serikali, wananchi na taasisi mbalimbali kwa ujumla wilayani humo zinapaswa kujitoa kwa moyo wa dhati na kuwekeza katika shughuli za upandaji miti.

No comments: