Sunday, December 13, 2015

SENYI NGAGA AWATAKA MADIWANI MBINGA KUTUMIKIA WANANCHI

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Venance Mwamengo upande wa kulia akizungumza jambo wakati wa  kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo, klichofanyika katika ukumbi wa Umati uliopo Mbinga mjini, kushoto ni Mwenyekiti  mpya wa Halmashauri hiyo, Ambrose Mtarazaki.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga vijijini mkoani Ruvuma, wametakiwa kujenga ushirikiano katika kusimamia na kukagua miradi ya maendeleo ya wananchi, ili iendane na thamani halisi ya fedha zinazotolewa na serikali. 

Aidha imeelezwa kuwa kutokana na baadhi ya Madiwani na watendaji wa serikali kutosimamia ipasavyo miradi hiyo, wamekuwa wakisababisha miradi mingi kutoendana na thamani halisi ya fedha iliyotolewa.

Madiwani wapya wa Halmashauri ya wilaya Mbinga vijijini wakila kiapo.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga alisema hayo wakati alipokuwa akiwasilisha salamu za serikali kwenye kikao cha baraza la Madiwani Halmashauri ya Mbinga vijijini, kilichoketi kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.

“Ndugu zangu, wenyewe mnaona kasi ya ufanyaji kazi kwa serikali hii ya awamu ya tano, watumikieni wananchi ipasavyo ili tuweze kuwaletea maendeleo mambo ya uchaguzi yamepita tuondoe tofauti zetu, sasa tunaingia katika utekelezaji kwa kufanya kazi za serikali”, alisema Ngaga.


Ngaga alieleza kuwa matarajio ni kuona madiwani na watendaji wake wa serikali, wanatimiza majukumu ya wananchi ipasavyo ili kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima, ambayo baadaye husababisha migogoro miongoni mwa jamii.

Pamoja na mambo mengine, katika kikao hicho cha baraza la madiwani waliweza kufanya uchaguzi wa kumchagua Mwenyekiti wao, atakayeweza kuongoza baraza hilo kwa kipindi cha miaka mitano.

Ambrose Nchimbi ambaye ni diwani wa kata ya Amani makolo, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliweza kushinda katika nafasi hiyo kwa kupata kura 37 huku akimbwaga chini mpinzani wake wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edmund Nditi aliyepata kura 1.

Hata hivyo kwa nafasi ya makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga vijijini, ilichukuliwa na Benuard Komba wa CCM ambaye alipita bila kupingwa.

No comments: