Wednesday, December 2, 2015

WAWILI WAPOTEZA MAISHA KATIKA MAPIGANO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI TUNDURU



Na Steven Augustino,
Tunduru.

WATU wawili ambao ni wakulima wanaoishi kijiji cha Tuliyeni, tarafa ya Nakapanya wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameuawa kikatili katika mapigano makali yaliyotokea kijijini hapo kati yao na wafugaji.

Taarifa za tukio hilo, zinaeleza kuwa chanzo cha mauaji hayo kilitokana na ugomvi na mgogoro mzito uliotokana kati ya wafugaji hao, ambao ni wa jamii ya Kimang'ati na wakulima hao. 

Kwa mujibu wa taarifa hizo, waliopoteza maisha katika tukio hilo wametambulika kwa majina ya Ahamad Matola (43) na Hamis Karlo (41) ambapo walidaiwa kuwa ndio wamiliki wa mashamba hayo, hivyo baada ya kuona ng'ombe akila mazao yao shambani ndipo walimshambulia kwa mapanga na kumkakata vipande na kugawana nyama yake.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walisema wakulima hao mara nyingi wamekuwa wakiwatuhumu wafugaji kuingiza mifugo yao katika mashamba yao na kwamba hata wakati wa kuswaga ng'ombe hao kurudi kutoka machungani, wamekuwa hawazingatii usalama wa mashamba ya wenzao.


Diwani wa kata ya Nakapanya,  Kubodola Ambali alisema kuwa tukio hilo lilitokea baada ya ng'ombe mmoja kuachwa nyuma na mchungaji wake ambapo baadaye aliingia katika mashamba ya wakulima hao na kushambulia mazao yao, jambo ambalo liliwafanya wamcharange kwa mapanga na kumchinja kisha kugawana nyama yake.

Alisema wakati wakulima hao wakiwa katika harakati hizo, wafugaji walirudi kwa lengo la kumfuatilia ng'ombe wao ambapo baada ya kushuhudia tendo hilo lililofanywa na wakulima hao, kugawana nyama ya ng'ombe wao ndipo wakacharuka na kuanzisha mapigano hayo.

Mganga aliyeifanyia uchunguzi miili ya marehemu hao, Dokta Joseph Ng'ombo alisema kuwa chanzo cha vifo hivyo, kilitokana na kutokwa na damu nyingi katika miili yao.

Dokta Ng'ombo aliendelea kufafanua kuwa pamoja na miili yao kukutwa ikiwa na alama za fimbo mwilini, katika tukio hilo marehemu Matola alitobolewa pia kwa mkuki na sime zaidi ya mara 12 katika sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela amethibitisha juu ya tukio hilo na kueleza kuwa tayari ametuma kikosi kazi kwenda katika eneo la tukio kwa ajili ya uchunguzi na kuhakikisha kwamba, wahusika wa tukio hilo wanakamatwa na kupelekwa katika vyombo vya sheria.

No comments: