Friday, December 18, 2015

GAMA: UNGENI MKONO MAGUFULI ANAVYO WASHUGHULIKIA WATENDAJI WABOVU

Baadhi ya waendesha boda boda ambao ni wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Songea wakisukuma gari la Mbunge wa jimbo la Songea mjini, Leonidas Gama mara baada ya mbunge huyo kuzungumza na vijana hao ambapo aliwataka kuendelea  kudumisha amani na utulivu, sambamba na kushiriki katika vita dhidi ya vitendo vya uhalifu wilayani humo. ( Picha na Muhidin Amri )


Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MBUNGE wa Jimbo la Songea mjini, Leonidas Gama amewataka vijana waliopo katika jimbo hilo kuunga mkono  jitihada mbalimbali zinazofanywa na Rais Dokta John Magufuli, juu ya namna anavyowashughulikia baadhi ya watendaji wabovu waliopo Serikalini ikiwa ni lengo la kuongeza kasi ya uwajibikaji kazi, katika maeneo yao ili Taifa liweze kukua kimaendeleo.

Gama alisema hayo juzi mjini Songea, alipokuwa akizungumza na waendesha pikipiki maarufu kwa jina la boda boda mara baada ya kumaliza kazi ya kufanya usafi, katika kata ya Ruhuwiko mjini hapa.

Alisema kuwa Watanzania wote wanakubali kwamba wamepata Rais bora, hivyo ni njia pekee sasa ya kuendelea kumuunga mkono ili aweze kukomesha vitendo vya rushwa, wizi na ufisadi vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa umma ambao sio waaminifu.


Vilevile alisema kuwa hatua hiyo  itasaidia kuharakisha ukuaji wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja, wilaya na taifa kwa ujumla kwa kile alichoeleza kuwa hivi sasa hata miradi ya maendeleo utekelezaji wake, utalingana na gharama halisi ya fedha zinazotolewa na serikali.

Alifafanua kuwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inatambua mchango mkubwa wa vijana wanaojishughulisha na biashara ya boda boda, ndiyo maana iliamua kuvunja sheria inayokataza chombo cha magurudumu mawili kubeba abiria ili vijana wengi wasiokuwa na kazi, wapate fursa ya kujiajiri kupitia boda boda na waweze kuwa na kipato.

Kupitia vikao vya Halmashauri ya Manispaa ya Songea, alisema atahakikisha wanafuta ushuru mdogo mdogo ambao ni kero kubwa kwa wafanyabiashara hasa akina mama wauza matunda na mboga mboga, kwani kero hiyo endapo itaachwa kwa muda mrefu huchangia kuwarudisha nyuma kiuchumi.

Mbali na hilo Gama alifafanua kuwa Madiwani wote wa  Manispaa hiyo, bila kujali itikadi za vyama vyao wamekubaliana  juu ya suala la kuinua uchumi wa mji huo kwa kuhimiza wananchi kutumia muda mwingi kufanya kazi za uzalishaji mali, kusimamia mapato na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha zinazokusanywa kutoka katika vyanzo mbalimbali.

Aidha ameahidi kwamba, atahakikisha anasimamia kikamilifu mikopo kwa vijana na wanawake ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ili waweze kujiinua kiuchumi, badala ya kuendelea kuwa tegemezi kwa watu wengine.

Hata hivyo amewaasa waendesha boda boda hao, kufuata sheria za usalama barabarani ikiwemo kuvaa kofia ngumu na kubeba abiria mmoja, kuacha kubeba wahalifu na kulisaidia Jeshi la Polisi kuwafichua watu wanaojihusisha na  vitendo  hivyo kama vile ukabaji, wizi wa kutumia silaha na hata wasichana wanaofanya biashara haramu ya ngono.

No comments: