Tuesday, December 22, 2015

UVCCM MBINGA WASHIRIKI JUKUMU LA KUFANYA USAFI


Wanachama wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wakishiriki katika zoezi la kufanya usafi.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANACHAMA wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamesema wataendelea kuunga mkono jukumu la kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya mji wa Mbinga, ili kuweza kuepukana na magonjwa yatokanayo na uchafu.

Aidha walieleza kuwa katika kuhakikisha kwamba jambo hilo linakuwa endelevu ndani ya mji huo, watahamasisha watu wengine kufanya hivyo na ni wajibu kwa kila mtu kuzingatia usafi katika eneo analoishi na sio kutupa taka hovyo.
 
Wanachama wa UVCCM wilayani humo, walisema hayo walipokuwa wakihojiwa na mwandishi wa habari hizi wakati walipokuwa wakifanya usafi kuzunguka Ofisi za CCM wilaya na maeneo mengine, ya uwanja wa mpira wa miguu ambao humilikiwa na chama hicho.

“Jukumu la usafi ni letu sote wananchi, sisi vijana tumeungana kwa pamoja kufanya kazi hii katika eneo hili, tunawaomba wananchi wengine watekeleze kwa vitendo suala hili ambalo ni muhimu mbele ya maisha yetu ya kila siku”, walisema.


Awali Katibu wa Umoja huo wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi wilayani Mbinga, Ally Simba ambaye alikuwa akiongoza kundi hilo la vijana kufanya usafi wa mazingira katika maeneo hayo, alisema kwamba wanamuunga mkono Rais John Magufuli kwa utendaji mzuri wa kazi ndani ya CCM ambao ameuonesha kwa kauli mbiu yake ya ‘hapa kazi tu’.

Simba alisema kuna kila sababu, kwa kila mtu kutekeleza majukumu muhimu ambayo yanaleta manufaa katika jamii kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho ikiwemo suala hilo la usafi, ambalo linapaswa kuzingatiwa kila siku.

Pia akielezea juu ya mikakati ya UVCCM wilayani Mbinga, alisema wanachama wa umoja huo wanapaswa kujenga ushirikiano wa pamoja na kuacha makundi yasiyokuwa ya lazima, ambayo yanaweza kuwagawa baadaye.

Hata hivyo aliongeza kuwa, mikakati mojawapo ya kuimarisha umoja wao ni kujenga ubunifu wa miradi ya kimaendeleo na kuendeleza iliyopo, kwa faida ya Chama na wanachama kwa ujumla.

No comments: