Sunday, December 27, 2015

WANANCHI WAIBUA MADUDU YALIYOPO HOSPITALI YA WILAYA MBINGA

Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

BAADHI ya wananchi wanaoishi katika Jimbo la Mbinga mjini mkoani Ruvuma, wamelalamikia juu ya kero wanazozipata katika Hospitali ya wilaya ya Mbinga mkoani humo, ikiwemo baadhi ya waganga kuwa na tabia ya kuomba rushwa kutoka kwa wagonjwa wanaokwenda hospitalini hapo kwa ajili ya kupata matibabu.

Rais John Pombe Magufuli.
Aidha imedaiwa kuwa kundi kubwa linaloathirika wanapokuwa katika hospitali hiyo ni la watoto wadogo na akina mama wajawazito, ambapo wanapokuwa kwenye foleni kwa ajili ya kumuona daktari hukaa muda mrefu bila kuhudumiwa na kusababisha wakati mwingine, mgonjwa kupoteza maisha.

Hayo yalisemwa na wananchi hao leo, kwenye mkutano maalumu ambao uliitishwa na Mbunge wa Jimbo hilo la Mbinga mjini, Sixtus Mapunda katika ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.

Mkazi mmoja wa kitongoji cha Lusonga aliyejitambulisha kwa jina la, Gerwada Nchimbi alieleza kuwa hata mama mjamzito ambaye amejifungua kwa njia ya operesheni endapo asipotoa rushwa ya fedha, dawa za kusafishia kidonda hapati na anaambiwa akanunue kwenye duka la dawa muhimu ndipo ahudumiwe.


“Mheshimiwa Mbunge, hata siku ya mwisho mama huyu anapotakiwa kufungua nyuzi za kidonda chake hawezi kupata huduma mpaka atoe kitu kidogo kwa mganga anayemkuta siku hiyo, tunaomba shughulikia haya ili tuweze kundokana na kero hizi”, alisema Nchimbi.

Naye Rose Ndunguru mkazi wa mjini hapa, aliongeza kuwa hata kwa upande wa wodi ya watoto, waganga wanaokuwa zamu wamekuwa wakitoa lugha mbaya kwa wagonjwa na wauguzi wao ambao wamelazwa katika hospitali hiyo ya wilaya ya Mbinga.

“Sisi tumechoshwa na hali hii, hawa watumishi wa idara ya afya hivi hawaridhiki na mishahara wanayopata, sisi wanyonge tunaonewa sana muda mwingine tukishapatiwa matibabu na mganga tunaambiwa………….wewe mama bado unadaiwa hela ya soda”, alisema Ndunguru.

Kwa upande wake akitolea ufafanuzi juu ya kero hizo, Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini, Mapunda alisema kuwa atakwenda kuonana na uongozi husika na kuona namna gani matatizo hayo yanatafutiwa ufumbuzi ili yasiendelee kuwepo.

“Ndugu zangu kweli Mbinga tunachangamoto kubwa juu ya hospitali yetu, tunahitaji pia kuwepo na vifaa tiba na madawa ya kutosha, tunahitaji kuendelea kushirikiana ili tuweze kumaliza matatizo haya yaliyopo”, alisisitiza Mbunge huyo.

No comments: