Tuesday, December 15, 2015

TUWEMACHO TUNDURU WAIPONGEZA TASAF KWA UJENZI WA ZAHANATI

 Mshauri na mfuatiliaji wa miradi ya TASAF wilayani Tunduru, Christian Amani aliyechuchumaa akishirikiana na fundi mshauri wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Hamisi Mpinda wakihakiki kwa kupima kiwango cha ukubwa wa tofari zinazofyatuliwa ili kufanikisha ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Tuwemacho iliyopo wilayani humo.                                           (Picha na Steven Augustino)


Na Steven Augustino,
Tunduru.

WANANCHI waishio katika kijiji cha Tuwemacho kata ya Tuwemacho wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameipongeza serikali kwa uamuzi wa kuwajengea zahanati kijijini humo ambayo wanaimani kwamba itawakomboa na adha waliyoipata kwa muda mrefu sasa, juu ya upatikanaji wa matibabu ya uhakika.

Mwenyekiti kijiji hicho, Sijaona Ally Pekani alibainisha hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ambaye alitembelea katika eneo hilo, kujionea ujenzi huo ambao unaendelea.

Pekani alifafanua kuwa kutokana na wananchi wake, kukabiliwa na kero hiyo kwa muda mrefu zaidi ya wananchi 2,000 kati ya wananchi wote 2,871 ambao wanaishi kijijini humo, wamejitokeza na kujitolea kuchangia nguvu zao juu ya ujenzi wa mradi huo wa zahanati.


Mtendaji wa kata ya Tuwemacho, Ipyana John alisema ujenzi wa mradi huo utasaidia kuwakomboa hata wananchi wanaoishi jirani kutoka vijiji vya Nasya, Tuwemacho, Chemchem na Namasalau ambavyo wakati wote hutegemea kupata huduma za matibabu katika Hospitali ya wilaya ya Tunduru ambayo ipo mbali nao.

Nao Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa mradi huo, Swalehe Ally Gemti na mjumbe wa kamati hiyo, Maua Yahaya walisema kwamba kukamilika kwa ujenzi wa mradi huo utakuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi hao na kuwaondolea kero ya kutembea kwa miguu umbali wa  zaidi ya kilometa 10, kufuata huduma za matibabu ambazo hupatikana Tunduru mjini.

Walisema toka kijiji hicho kianzishwe mwaka 1974 hadi leo hii, wananchi wamekuwa wakifuata huduma ya matibabu hospitali ya wilaya hiyo jambo ambalo limekuwa likisababisha baadhi ya wagonjwa kupoteza maisha, wakati wakiwa njiani kuelekea huko huku wakihatarisha pia usalama wa maisha yao kutokana na wanyama wakali waliopo katika misitu iliyopo katika njia za kuelekea mjini.

Mradi huo unajengwa kwa ufadhili wa  Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) hapa nchini, tofauti na awali ulikuwa unajengwa chini ya mfuko wa jimbo ambapo ulikwama kutokana na kukosekana fedha.

Akizungumza na mafundi wanaoendelea na kazi ya ujenzi huo, fundi mshauri wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru, Hamisi Mpinda aliwataka mafundi wenzake wanaoendelea na kazi hiyo kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na wataalamu pamoja na kufuata vipimo husika. 

Kadhalika naye mshauri na mfuatiliaji wa miradi ya TASAF wilayani humo, Christian Amani alisema mradi huo hadi kukamilika ujenzi wake, utagharimu kiasi cha shilingi milioni 75.

Hata hivyo alieleza kuwa katika kuhakikisha unajengwa na kukamilika kwa wakati, tayari mfuko huo wa maendeleo ya jamii umekwisha toa fedha zote na kilicho bakia ni utekelezaji na ukamilishaji wa kazi ya ujenzi huo.

No comments: