Wednesday, December 9, 2015

MWAMBUNGU AWAPA TANO MADIWANI WA TUNDURU



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma, wamemchagua Diwani wa kata ya Mchoteka, Mbwana Mkwanda Sudi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa Mwenyekiti wao wa Halmashauri hiyo, ili aweze kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano.

Aidha katika uchaguzi huo madiwani hao, pia walimchagua Diwani wa kata ya Namakambale kupitia tiketi ya CCM, Mfaume Wadali Khalifa  kuwa makamu wa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo.

Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Matokeo ya uchaguzi huo, yalitangazwa kwenye ukumbi wa Klasta ya walimu tarafa ya Mlingoti iliyopo mjini hapa. 

Msimamizi wa uchaguzi huo, Ghaib Lingo alisema kuwa katika matokeo hayo Mbwana alichaguliwa baada ya kupata kura 39 na kumbwaga mpinzani wake, Abdalah Rajab Abdalah aliyepata kura 16.

Kwa upande wa nafasi ya makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mfaume Wadali Halifa (CCM) alipata nafasi hiyo kwa kura 39 na kumbwaga mpinzani wake Alliasa Mohamed Mshamu kutoka Chama Cha Wananchi (CUF) aliyepata kura 16.


.
Wakitoa neno la shukrani kwa nyakati tofauti Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ya Tunduru, Mbwana Mkwanda Sudi na Makamu wake, Mfaume Wadali waliahidi kutoa ushirikiano kwa madiwani na wataalamu wote katika kuhakikisha kwamba wilaya hiyo inasonga mbele kimaendeleo.

Katika utekelezaji wa shughuli zao za usimamizi wa maendeleo, walisema hawatakuwa na ubaguzi wala upendeleo wa aina yeyote ile kwani kufanya hivyo wanaamini watajenga makundi yasiyokuwa ya lazima ndani ya wilaya, na kuleta mipasuko miongoni mwa jamii.

Akizungumza katika mkutano huo wa kuzindua baraza hilo la Madiwani, Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu aliwaasa madiwani ambao waliingia katika baraza hilo kwa tamaa ya kutaka kupata fedha, kwamba safari hii hakuna fedha na wanachotakiwa ni kuwatumikia wananchi.

"Kama wapo viongozi ambao wamepata udiwani kwa lengo la kutekeleza vitendo vyao vya uporaji, ulafi na wizi wa fedha serikali ya awamu ya tano chini ya Dokta John Magufuli hawatapata nafasi ya kufanya vitendo hivi", alisema Mwambungu.

No comments: