Thursday, December 24, 2015

HOSPITALI WILAYA YA MBINGA YAKABILIWA NA TATIZO LA UCHAKAVU JENGO LA UPASUAJI, SIXTUS MAPUNDA ASISITIZA KUJENGA USHIRIKIANO KUTATUA MATATIZO YALIYOPO

Sixtus Mapunda Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini upande wa kulia, akikabidhi vifaa tiba kwa Mganga mkuu wa Hospitali ya Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, Elisha Roberth ambapo zoezi hilo la makabidhiano hayo lilifanyika katika hospitali ya wilaya hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini, Sixtus Mapunda akiwagawia miswaki, dawa za kusafishia meno na sabuni za kuogea akina mama wajawazito ambao wanasubiri kujifungua waliopo Hospitali ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.
Sixtus Mapunda, akizungumza na akina mama wanaosubiri kujifungua katika wodi ya wazazi iliyopo Hospitali ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma. (Picha zote na gwiji la matukio Ruvuma)
Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

HOSPITALI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa jengo la kisasa la upasuaji jambo ambalo wagonjwa wengi wanaohitaji kupata huduma za upasuaji katika hospitali hiyo, hupata shida kutokana na jengo linalotumika sasa kuwa chakavu na halikidhi mahitaji husika.

Aidha imeelezwa kuwa hospitali hiyo, haina gari la kubebea wagonjwa ambapo hulazimika kutumia gari la kituo cha afya Mapera, kilichopo katika kata ya Mapera wilayani humo.

Sixtus Mapunda ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini, alielezwa hayo leo alipokuwa katika ziara ya kutembelea hospitali hiyo ya wilaya Mbinga kwa lengo la kujionea changamoto mbalimbali, ambazo hospitali hukabiliana  nazo.

Aliweza kutoa mchango wa vifaa tiba kama vile dawa za kufanyia usafi, bandeji za kufungia na kusafishia vidonda na mipira ya kuvaa mikononi (Gloves).
 
Vilevile aliwapatia akina mama wajawazito na waliojifungua watoto ambao wapo wodini wamelazwa; sabuni za kuogea, miswaki na dawa za kusafishia meno ikiwa ni lengo la kuboresha afya zao ziweze kuwa katika hali nzuri.


Mbunge huyo ambaye aliambatana na mkewe, Jiang Alipo walikutana na changamoto kadhaa ambazo hospitali hiyo hukabiliana nazo, ikiwemo uchakavu wa majengo hasa la akina mama hao wajawazito na wagonjwa mahututi (ICU).

Akisoma taarifa fupi juu ya maendeleo ya hospitali ya wilaya ya Mbinga, Mganga mkuu wa halmashauri ya mji wa Mbinga, Dokta Elisha Roberth alisema kuwa jengo la kulaza wagonjwa daraja la kwanza lililopo katika hospitali hiyo, hasa kipindiki hiki cha masika linavuja na kwamba linahitaji ukarabati mkubwa ili liweze kuwa katika hali nzuri.

“Licha ya kuwepo na changamoto nyingi zinazotukabili, wodi ya wazazi pia ni chakavu inahitaji ukarabati ili hata mbu ambao huingia katika madirisha ambayo ni mabovu na kuleta madhara kwa wagonjwa, wasiweze kuendelea kuleta matatizo”, alisema Dokta Elisha.

Dokta Elisha alizungumzia pia tatizo la uhaba wa watumishi, alisema kuwa wagonjwa wanaotakiwa kupatiwa matibabu ni wengi hivyo kuna kila sababu kwa serikali kuona namna ya kutatua tatizo hilo, ili wagonjwa waweze kupatiwa huduma ipasavyo.

“Upungufu wa watumishi nilionao ni mkubwa hasa kwa kada ya madaktari, wagonjwa tunaowapokea kwa siku ni wengi hufikia idadi ya 180 hadi 210 lakini tunafanya jitihada pamoja na upungufu wa watumishi tulionao tunatekeleza majukumu tunayopaswa kuyatekeleza”, alisema.

Pamoja na mambo mengine, Mganga huyo aliongeza kuwa kumekuwa na tatizo la kutokuwepo kwa jengo la kutolea huduma wagonjwa wenye matatizo ya akili ambapo hivi sasa hulazimika kulaza wagonjwa wenye matatizo hayo, katika wodi za wagonjwa wengine wa kawaida jambo ambalo wakati mwingine waganga wanaokuwa zamu kutibu wagonjwa wodini, huogopa na kutotimiza majukumu ya kazi zao ipasavyo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini, Sixtus Mapunda baada ya kupokea changamoto hizo aliahidi kujenga ushirikiano kati ya uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo (serikali) na wadau mbalimbali, juu ya kutatua kero hizo na hatimaye wananchi waweze kupata huduma kikamilifu.

“Ni lazima tujenge ushirikiano mkubwa ili tuweze kutatua matatizo haya yaliyopo mbele yetu, tusitegemee wakati wote tupate mahitaji kutoka wizara ya afya naomba tushirikiane ili tuweze kutimiza malengo husika”, alisema Mbunge huyo.

Hata hivyo, Mapunda alisema yeye anatambua kwamba sekta ya afya inakabiliwa na changamoto nyingi hivyo amewataka wafanyakazi wote kwa ujumla wao waliopo katika hospitali ya wilaya ya Mbinga, kutekeleza wajibu wao ili kuweza kutimiza matakwa husika ya wananchi na kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima miongoni mwa jamii.

No comments: