Wednesday, December 9, 2015

MBUNGE CHADEMA TUNDURU ASHINDWA KUHUDHURIA KIKAO KUTOKANA NA KUKOSA BARUA YA UTAMBULISHO


Na Steven Augustino,

Tunduru.

MBUNGE wa viti maalum, Zubeda Hassan kupitia tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alishindwa kuhudhuria kikao cha kwanza cha kuwaapisha Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, kutokana na Mbunge huyo kutofika na barua ya utambulisho kutoka makao makuu ya chama hicho.

Msimamizi wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Ghaib Lingo alitoa ufafanuzi huo mbele ya Madiwani wote wa wilaya hiyo, ambao walihudhuria katika kikao hicho.

Akifafanua taarifa hiyo, alisema hali hiyo imekuja kwa lengo la kutaka kujiridhisha juu ya uhalali wa kuteuliwa kwake na chama chake na hawatambui kuwa ni Mbunge wa jimbo gani, kati ya Tunduru Kaskazini au Kusini.


Aidha aliwatoa hofu kuwa, Mbunge huyo ambaye pia serikali inaamini kuwa ameteuliwa kihalali, atatambulishwa kwa Madiwani hao katika vikao vijavyo mpaka barua yake ya utambulisho itakapowasilishwa katika Halmashauri hiyo.

Katika mchakato wa uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu, jumla ya vyama vitatu vilisimamisha wagombea wake wa ubunge katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.

Lingo alivitaja vyama vilivyosimamisha wagombea wa nafasi hiyo, ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama Cha Wananchi (CUF) kupitia  Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na chama cha ACT Wazalendo.

No comments: