Wednesday, December 2, 2015

WAKULIMA TUNDURU KUNUFAIKA NA UBANGUAJI BORA WA KOROSHO

Mtambo wa kubangua na kuchambua korosho uliopo katika kiwanda cha kubangulia korosho wilayani Tunduru, mkoa wa Ruvuma.


Na Steven Augustino, 

SIKU zote Taifa la Tanzania limekuwa likitegemea kilimo kuwa ndio uti wa mgongo, hivyo bila  uwepo wa viwanda vya kusindika mazao ambayo yamekuwa yakizalishwa na wakulima hao, uzalishaji wao utakuwa ni kazi bure na hauwezi kuwaletea tija katika maisha yao.

Kutokana na uwepo wa umuhimu wa sekta ya viwanda hapa duniani katika kukuza uchumi na kuhakikisha dhamira hiyo inatimia, umoja wa kundi la Export Trading  Group (ETG)  umechukua jukumu la kupeleka fursa ya ujenzi wa kiwanda cha kubangulia zao la korosho kwa wakulima wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.

Ni ukweli usiofichika kwamba,  kiwanda hiki ambacho ni tegemeo  kubwa katika kuinua uchumi wa wananchi wa wilaya hiyo, hivi sasa kimejiwekea mikakati kabambe ambayo itaenda sambamba na msimamo wa serikali ya awamu ya tano  inayoongozwa na Dokta John Pombe Magufuli, ambaye amekuwa akitilia mkazo wa kufufua na kujenga viwanda vipya hapa nchini, ili kuweza kuongeza ajira.


Kiwanda hiki ambacho kinaendeshwa chini ya mwamvuli wa kundi la  (ETG) ambalo ilikinunua, wakati kinamilikiwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pale ilipojitoa katika uwekezaji mwaka 2005.

Baada ya kukamilika kwa taratibu hizo ETG, ilianza utekelezaji wa shughuli za ubanguaji korosho kutoka kwa wakulima wa wilaya hiyo, mwezi Aprili  mwaka 2008 na kwamba hivi sasa kimekuwa tegemeo kubwa la kutoa ajira kwa wananchi wa wilaya ya Tunduru.

Takwimu kutoka ndani ya uongozi wa kiwanda hiki, ambazo zimethibitishwa na mhasibu wa kiwanda hicho, Niraj Patel zinaeleza kuwa jumla ya watu 700 kutoka idadi ya watu 300 wameweza kuwaajiri wakati kinaanzishwa.

Anasema mbali na mafanikio hayo na kufikia idadi ya kutoa ajira hizo, wengi wao walioajiriwa ni wanawake ambao hivi sasa wamekuwa wakinufaika na familia zao ambazo wanaishi nazo.

Pamoja na watu hao kuishi katika kipindi hicho na kutegemea ajira  za muda, anasema kwamba wamekuwa pia wakinufaika kutokana na kipato ambacho hutokana na ujira huo, kwa kujiletea maendeleo.

"Sisi kama kiwanda hatuwatazami watu 700, wanaofanya kazi katika kiwanda chetu, bali tunawahudumia kwa kuzitazama familia zao ambazo zinawazunguka wafanyakazi wetu", alisema Patel.

Anasema uwekezaji wa kiwanda hiki wilayani hapa, unalenga kuongeza ajira mbadala kwa jamii pamoja na uzalishaji wa zao la korosho hapa nchini, kuboresha upatikanaji wa soko bora na la uhakika kwa zao hilo, pamoja na kutangaza jina la Tanzania.

"Uwekezaji wa kiwanda chetu mbali ya kutegeneza ajira mbadala kwa jamii, pia tunalenga kuongeza uzalishaji wa zao hili la Korosho na upatikanaji wa masoko ya uhakika ya kuuzia zao hili", alifafanua Patel.

Shughuli zinazofanywa katika kiwanda hicho anasema kuwa zinajumuisha ununuaji wa zao hilo, ukaushaji, ubanguaji, upangaji wa madaraja, upakiaji na uuzaji wa korosho hizo nje ya nchi. 

Katika kufikia lengo husika uongozi wa kiwanda, umekuwa ukiangalia uwezekano wa kuanza kutoa ajira ya kudumu miongoni mwa wafanyakazi wake, ikiwa ni juhudi ya uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi wake.

Naye fundi mkuu wa mitambo katika viwanda vya kubangulia zao la korosho wilayani Tunduru, Masasi, Newala na Mtwara Injinia Sivan Edayeth anasema pamoja na kuwepo kwa mafanikio hayo, bado wanahitaji kuendelea kuboresha miundombinu ya viwanda vilivyopo katika maeneo hayo.

Injinia huyo anasema lengo uboreshaji huo, ni kuweza kurahisisha uzalishaji wa korosho kuwa katika ubora wa hali ya juu na unaokubalika.

Anasema hivi sasa mitambo iliyopo katika kiwanda cha Tunduru, inao uwezo wa kuzalisha kiasi cha tani  4,000 katika kipindi cha misimu tofauti na hapo awali walikuwa wakibangua tani 2500.

Utekelezaji wa shughuli zao, kiwanda hutegemea kuuza korosho katika masoko yaliyopo katika nchi ya India, Marekani, Uingereza na zile za ukanda wa ghuba. 

Mhandisi Edayeth anawashukuru viongozi wa serikali na wananchi wa wilaya ya Tunduru, kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiwapatia tangu kuanzishwa kwa kiwanda hicho.

Kadhalika msimamizi mkuu wa wafanyakazi wa kiwanda hicho, Issa Kaesa anaeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa kiwanda hicho kumekuwa kukijitokeza malalamiko mbalimbali, kutoka kwa wafanyakazi wake lakini kutokana na uhodari wa uongozi wao wamekuwa wakiyatatua na kuendelea na kazi.

No comments: