Wednesday, December 30, 2015

HALMASHAURI MADABA YAKAMILISHA UPIMAJI VIWANJA 500



Na Mwandishi wetu,
Songea.

HALMASHAURI ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, imekamilisha mradi wa upimaji viwanja 500 katika kijiji cha Madaba  wilayani humo, ambavyo vitatumika kwa ajili ya ujenzi wa mji mpya wa wilaya hiyo.

Upangaji  mpya wa eneo hilo, umeanza na upimaji viwanja katika maeneo ambayo wananchi wanayatumia kama  mashamba ambapo wametakiwa kuyaachia ili kupisha kazi  hiyo, hatua inayotajwa kwamba itaweza kubadili sura ya  wilaya hiyo mpya na kuwa mji mdogo.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmshauri hiyo, Robert Mageni alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa upangaji mpya wa eneo  la kijiji cha Madaba na maeneo jirani, utazingatia ramani itakayochorwa na wataalamu husika kutoka idara ya ardhi.


Alisema kuwa kutokana na uboreshaji wa eneo hilo, baadhi ya maeneo yatachukuliwa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo huduma za afya, kituo cha Polisi na mabasi likiwemo pia soko la kisasa na kwamba wananchi wanaomiliki maeneo hayo watalipwa fidia.

Kwa mujibu wa Mageni alieleza kuwa kutokana na hatua hiyo, viwanja vingine vitauzwa kwa watu binafsi, taasisi za serikali na mashirika ya dini ambapo tayari Kanisa katoliki Jimbo la Njombe limeonesha kuhitaji maeneo, kwa  ajili ya ujenzi wa vitega uchumi katika kijiji hicho.

Alisema kuwa watu na taasisi zitakazopewa viwanja hivyo, watatakiwa kujenga nyumba za kisasa na kufanya uwekezaji wa aina mbalimbali, ikiwa ni lengo la kufanya Madaba uwe mji mzuri wa kibiashara.

“Tunatambua umuhimu wa shughuli za kilimo zinazofanywa na wananchi wetu katika eneo hili, hata hivyo tunawaomba wananchi watusamehe kutokana na  usumbufu utakaojitokeza kwani kila kitakachotekelezwa ni kwa manufaa ya watu wote”, alisema Mageni.
 
Aliongeza kuwa, uboreshaji huo utawezesha wananchi kupata huduma muhimu   kwa urahisi kama vile maji safi na salama, miundombinu ya barabara, umeme wa uhakika ambao utaunganishwa na gridi ya Taifa unaoendelea kujengwa kutoka Makambako  hadi Songea kupitia wilaya hiyo ya Madaba.

No comments: