Friday, December 18, 2015

BASI LA NEW FORCE LAPATA AJALI MKOANI IRINGA LEO 12 WAPOTEZA MAISHA 28 WAJERUHIWA VIBAYA

Basi lililopata ajali la kampuni ya New Force lenye namba za usajili T 483 CTF
IRINGA.

WATU 12 wamefariki dunia na wengine 28 kujeruhiwa vibaya, ambao ni abiria waliokuwa wakisafiri baada ya basi walilopanda, mali ya kampuni ya New Force lililokuwa likitokea Dar es Salaam kulekea Tunduma Mbeya kugongana na roli lililokuwa likitokea Mafinga mkoani Iringa, likielekea Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, ACP Peter Kakamba amethibitisha kwa njia ya simu kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa ajali ilitokea majira ya 7.30 mchana katika eneo la Igeme kata ya Mahenge, wilayani  Kilolo mkoani Iringa.

Alisema ajali hiyo ilitokea baada ya lori hilo lenye namba za usajili, T 616 BEF aina ya SCANIA lilokuwa na tela namba T 320 BEF kupasuka tairi la mbele na hatimaye kulivaa basi hilo lenye namba T 483 CTF. 


Majina ya watu waliofariki, ambao kati yao wanaume wako nane na wanawake wanne hayakuweza kupatikana mara moja na kwamba utambuzi unaendelea.

Aliwataja majeruhi waliokimbizwa katika Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa kuwa ni pamoja na Michael Mahenge (40), Hawadi Msigwa (27) na Eliud Kalinga (20) wote wakazi wa Tunduma, Nicholaus Charles (45) mkazi wa Dar es Salaam,  Lulu Norbeth (15) na Anton Mwashiuya (43) wakazi wa Mbozi, Mbeya.

Wengine ni  Juma Wiliam Lucas Wilian, Willson Ndumba, Anitha Obadia Sanga, Arapha Hamdan, Razak Ngai na James Duma (49) raia wa Afrika Kusini.
 
Majeruhi wengine ni Jonas, Kasungu Kabanga raia wa Congo, Frank Kalinga, Silverster Ndenye, Aizack Ndula, Lulu Ndula na Suma Japhet.

Kadhalika mganga Mkuu mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa, Dokta Useleta Nyakiroto amethibitisha kupokea miili ya marehemu na majeruhi.

“Tumepokea miili ya marehemu 12 na tunaendelea  kufanya utambuzi wa majeruhi 28 ambao pia tunaendelea na utambuzi wao”, alisema Nyakiroto.

Hata hivyo miili ya marehemu hao, imehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali hiyo na majeruhi wanaendelea na matibabu, hali zao zitapoonekana kuimarika wataruhusiwa kwenda makwao. 

No comments: