Tuesday, December 15, 2015

MAGUFULI APONGEZWA KWA UTENDAJI KAZI IMARA NA SHUPAVU



Na Julius Konala,
Songea.

WAENDESHA pikipiki maarufu kwa jina la boda boda, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamempongeza Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Magufuli kutokana na utendaji kazi wake imara na shupavu.

Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa waendesha boda boda Manispaa ya Songea mkoani humo, Abeid Nchimbi kwa niaba ya wenzake alipokuwa akisoma risala yao mbele ya mgeni rasmi Mbunge wa jimbo la Songea mjini Leonidas Gama, ambalo lilipambwa na maandamano ya pikipiki kutoka Ruhuwiko na kisha kupokelewa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, kwenye uwanja wa michezo Majimaji uliopo mjini hapa.
Leonidas Gama.

Nchimbi alisema kuwa wameamua kumuunga mkono kutokana na jitihada zake anazo zionesha katika kupambana na vita dhidi ya rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya fedha za serikali, wanaokwepa kulipa kodi pamoja na kukamua majipu mengine mbalimbali.

Aidha alisema kuwa kutokana na imani kubwa aliyoionesha Dokta Magufuli kwa Watanzania, hivyo wao kama vijana wameamua kuvunja makundi mbalimbali yaliyokuwa miongoni mwao na kuamua kujiunga katika vikundi vidogo vidogo vya uzalishaji na ujasiriamali, kwa lengo la kujikwamua na hali ngumu ya maisha.


Akizungumza katika tukio hilo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea mjini, Gerlod Mhenga amewataka vijana hao kuendelea kukiunga mkono chama hicho na kumuomba Mbunge wa jimbo la Songea mjini, Leonidas Gama kuhakikisha anatekeleza ahadi mbalimbali alizowaahidi wananchi wake, wakati wa kampeni zilizopita za uchaguzi mkuu ikiwa pamoja na kutoa mikopo katika vikundi vya  akina mama na vijana, hususani kwa hao waendesha boda boda.

Naye Mkuu wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Benson Mpesya amewapongeza vijana hao kwa kuendelea kufanya usafi wa mazingira, kuzoa taka kwenye maghuba mbalimbali huku akiwataka waendelee na moyo huo wa kizalendo.

Kwa upande wake Mbunge huyo wa jimbo la Songea mjini kupitia tiketi ya CCM alisema, atahakikisha akina mama na vijana wanapatiwa mikopo yenye riba nafuu kwa lengo la kupanua ajira, kuongeza mzunguko wa fedha na kuimarisha uchumi wao huku akiwataka kuendelea kumuunga mkono Dokta Magufuli kwa kufanya kazi halali kwa juhudi na maarifa, kuwafichua mafisadi, majambazi na kufuata sheria za usalama barabarani.

No comments: