Thursday, December 17, 2015

WANAOJIHUSISHA NA UHARIBIFU WA MAZINGIRA WACHUKULIWE HATUA



Na Mwandishi wetu,
Songea.

WATENDAJI wa vijiji na kata wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, wameagizwa kuwakamata na kuwachukulia hatua kali watu wote wanaojihusisha na uchafuzi wa mazingira na uharibifu wa vyanzo vya maji katika maeneo yao.

Agizo hilo limetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Sigsbert Kaijage wakati alipokuwa akifunga kikao cha siku moja cha Wadau wa zao la muhogo, kilichoandaliwa na Muunganisho wa Vikundi vya Ujasiriamali Vijijini (MUVI) kwenye ukumbi wa Chuo kikuu huria uliopo mjini hapa.

Kadhalika ameagiza kutumia sheria ndogo za Halmashauri,  ili kuweza kuwabana na kuwafikisha Mahakamani watu wanaojihusisha na uchomaji misitu hovyo ambao wamesababisha baadhi ya maeneo mkoani humo, kuanza kugeuka jangwa na kupungua kwa kiwango cha mvua.


“Watu wanaochoma moto na uharibifu wa mazingira katika maeneo yetu tunawatambua, tutumie sheria zilizopo kuwafikisha Mahakamani kwani tayari athari zimeanza kuonekana juu ya uharibifu huu ambao unaendelea kufanyika”, alisema Kaijage.

Alisema kuwa hali ya mazingira katika  maeneo mengi  ya mkoa wa Ruvuma, yameharibiwa kutokana na kasi kubwa ya uchomaji moto misitu jambo ambalo linatishia mkoa huo, kuanza kugeuka kuwa jangwa na kupotea kwa vyanzo asili vya maji na wanyama ambao wanatumika kwa ajili ya utalii wa ndani.

Watumishi wa serikali amewataka kutambua kwamba, wao ndiyo jicho la wananchi hivyo ni vyema wawe mfano bora na wakuigwa kwa kuendelea kuelimisha jamii, juu ya kuachana na vitendo vya uharibifu huo wa mazingira.

No comments: