Sunday, December 20, 2015

UWT MBINGA YAONYWA



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga. 

WANACHAMA wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuacha malumbano miongoni mwao badala yake wajenge mshikamano na kuwa pamoja, ili waweze kusonga mbele kimaendeleo. 

Aidha imeelezwa kuwa endapo wataendekeza hali hiyo, majungu na fitina hayatawafikisha mbali ndani ya umoja huo jambo ambalo litasababisha waendelee kufarakana na kujenga makundi ambayo yatawagawa na kuleta mpasuko kati yao.

Rai hiyo ilitolewa na Katibu wa UWT wilaya ya Mbinga, Martina Katyale alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, juu ya maendeleo ya Umoja huo wa wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani hapa.


Katibu huyo alieleza kuwa wakati umefika sasa kwa wanawake wilayani humo, kujishughulisha na kazi za ujasiriamali ili waweze kuepukana na mambo hayo na kuwafanya wakue kiuchumi, kutoka ngazi ya familia zao na chama kwa ujumla.

“Nawasihi wanawake wenzangu tuachane na tabia ya kutengenezeana maneno ya hapa na pale ambayo hayatatujenga, mifarakano au matatizo yoyote yale yanayojitokeza katika jamii, hayawezi kuleta amani bali hujenga chuki na kuondoa upendo miongoni mwetu”, alisema Katyale.

Katyale alisisitiza kwamba wanachotakiwa wajiulize kwanza wametoka na wanakwenda wapi, huku wakiacha tabia za unafiki na uongo vitendo ambavyo kama wataviendekeza havitawafikisha mbali.

Katibu huyo wa UWT alifafanua kuwa Tanzania ni nchi ambayo wanawake wamekuwa wakipendana, hivyo chama kilichopo madarakani hakitakubali kuiacha rehani kwa watu wabovu ambao hawana nia njema na taifa hili.

Pamoja na mambo mengine, aliongeza kuwa Umoja huo wa Wanawake hauendeshwi kwa mtindo kama vile wa kucheza bao, hivyo wameshauriwa kuwa makini na majukumu ya kazi zao za kila siku katika kutumikia wananchi huku akiongeza kwa kuwataka wanachama wenzake, kuwabeza watu ambao wakati wote wamekuwa wakipinga maendeleo pale yanapofanyika.

No comments: