Monday, December 7, 2015

MADIWANI TUNDURU WATAKIWA KUMALIZA TOFAUTI ZAO



Na Steven Augustino,
Tunduru.

SERIKALI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, imewataka Madiwani wake  kumaliza tofauti zao za  kisiasa ili waweze kuisaidia Halmashauri yao ya wilaya, kusukuma mbele maendeleo ya wananchi waliowachagua.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa muda ambaye aliteuliwa kusimamia shughuli za kuwaapisha madiwani hao, ambaye ni Katibu tawala wa wilaya ya Tunduru Ghaib Lingo, wakati akifungua kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Klasta ya walimu tarafa ya Mlingoti mjini hapa.

Lingo alisema endapo madiwani watashindwa kuvua makoti ya itikadi za vyama vyao ambavyo viliwafanya kuingia madarakani, upo uwezekano mkubwa wa wilaya hiyo kutopiga hatua mbele za kimaendeleo.


Huku wakiongozwa na Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya wilaya hiyo, Gladys Nancy Barthy  katika kula viapo vyao vya udiwani madiwani wote waliahidi kuwatumikia wananchi kwa moyo na nguvu zao zote, kwa kufuata kanuni na miongozo iliyowekwa na serikali.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, nao wabunge wa majimbo ya Tunduru Kusini Daimu Idd Mpakate, Tunduru Kaskazini Mhandisi Ramo Matala Makani na Mbunge wa viti maalum Sikudhani Chikambo kwa pamoja waliwataka madiwani hao kuunganisha nguvu zao, ili kufanikisha utekekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo. 

Mbunge wa viti maalum, Sikudhani Chikambo pamoja na kuwapongeza madiwani hao aliwaomba kuimarisha umoja wao na kuachana na ushabiki wa vyama ambao hautaweza kuwasaidia, katika kuwaletea maendeleo wananchi walio wachagua.

Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, Daimu Mpakate alisema hivi sasa wanayo kazi ngumu ya kutekeleza matakwa ya wananchi walio wachagua, hivyo inabidi wajipange na kuhakikisha kwamba maendeleo yaliyotarajiwa yanafanikiwa kwa wakati. 

Mbunge wa jimbo la Tunduru Kaskazini, Mhandisi Ramo Makani aliwataka kurejea na kufanya kwa vitendo utekelezaji wa maendeleo ya wananchi na kwamba utekelezaji huo ulenge kushughulikia, kero zinazowakabili wananchi wao.

No comments: