Monday, December 21, 2015

DIWANI CHADEMA AKATAA POSHO ZA VIKAO



IRINGA.

DIWANI wa kata ya Gangilonga, Iringa mjini kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Daddy Igogo amesema hatapokea posho za vikao vyote vya baraza la madiwani katika kipindi chake cha miaka mitano, badala yake ametaka zitumike kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika kata yake.

Diwani huyo mdogo kuliko madiwani wote wa Halmashauri hiyo, ambaye pia ni Mwalimu katika Chuo Kikuu cha Ruaha, Iringa anakuwa diwani wa kwanza  nchini kukataa posho hizo huku baada ya Mbunge wa Singida Magharibi,  Elibariki Kingu (CCM) naye kukataa kupokea posho kama hizo katika kipindi chote atakachokuwa mbunge wa jimbo hilo. 

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya kata ya Gangilonga, ambapo  Igogo alisema kuwa ameamua kuchukua uamuzi huo ili kusaidia yatima na kuunga mkono ilani ya chama chake ya uchaguzi wa 2010 na 2015 ya kukataa posho ya vikao na kwamba, amekwisha muandikia barua mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo, inayompa maelekezo ya wapi posho hizo zipelekwe.


Igogo alisema kuwa posho za vikao ni ugonjwa wa ufisadi unaolitafuna taifa kila kukicha hususan kwa watendaji wa mashirika ya umma, watendaji wa serikali kuu na kumpongeza Rais  John Magufuli kwa kubana matumizi yasiyo ya lazima kwa fedha nyingi, na zaidi zielekezwe katika miradi ya maendeleo.
 
Alisema posho za wabunge zinalingana na bajeti ya sense, ambapo Taifa lilikwenda kukopa baadhi ya fedha ili kuendeshea zoezi hilo huku wastani wa posho kwa madiwani na watendaji katika Manispaa ya Iringa, kwa mwaka zinauwezo wa kusomesha zaidi ya wanafunzi 400 wa shule za sekondari kwa ada ya shilingi eflu 20,000 kwa kila mmoja na fedha zitabaki.

Kadhalika Diwani huyo aliwaomba madiwani wa chama chake na mbunge wa Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa na wabunge wote wa viti maalum kuwa sehemu ya kupinga uendelezwaji wa posho zisizo za msingi, ili kuonyesha dhamira ya dhati katika kuwatumikia watanzania.

Hata hivyo katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo wilaya ya Iringa mjini ambaye pia ni diwani wa kata ya Mivinjeni, Frank Nyalusi alisema uamuzi aliochukua diwani huyo ni mzuri na ni maamuzi yake ila yeye hana mpango wa kugomea kuchukua posho hizo.

No comments: