Tuesday, February 23, 2016

ASKOFU MKUU JIMBO LA MBINGA AWATAKA WATENDAJI WA SERIKALI KUENDANA NA KASI YA UTAWALA WA MAGUFULI

Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

ASKOFU Mkuu wa Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma, John Ndimbo ameeleza kuwa Watendaji waliopo katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani humo, wametakiwa kuwa tayari kupokea majukumu yanayoendana na nafasi walizonazo ikiwemo, kasi ya utawala wa serikali ya awamu ya tano kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.

“Kumbukeni, vigezo vya Rais wetu John Magufuli anavyovitaka katika nchi yetu ili iweze kusonga mbele ni kuwa wazalendo kwa mali zetu, kwa manufaa ya wananchi”, alisema Ndimbo.

Askofu John Ndimbo.
Kadhalika alibainisha kuwa viongozi wanapopanga mambo ya kimaendeleo, wanapaswa kushirikisha watu waliopo katika eneo husika na sio kufanya peke yao kwa kukaa mezani na kutengeneza mambo ambayo siku ya mwisho, yamekuwa yakileta kero na kuzua migogoro isiyokuwa na tija.

Askofu Ndimbo alieleza hayo jana alipokuwa akihutubia kwenye kikao cha baraza la Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Mbinga, lililofanyika mjini hapa katika ukumbi wa Umati huku akiongeza kuwa kiongozi ambaye hatimizi majukumu yake ipasavyo, anapaswa kujiondoa mapema kabla ya kutokea madhara kwa watu anaowatawala.

Pia alitolea mfano kwa kueleza kwamba, kuna baadhi ya watendaji wa vijiji na kata ambao wamepewa dhamana ya kuongoza wananchi katika maeneo yao wamekuwa hawatekelezi na kufuata taratibu za nchi kama zinavyotaka, hivyo alishauri wachukuliwe hatua mapema ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.


“Matumizi mabaya ya madaraka tuyaache, tukizingatia hili hata rungu la kuwajibishwa na viongozi wa juu waliopo katika serikali yetu tutaepukana nalo, tufanye kazi kwa juhudi na maarifa, ili tujijengee historia nzuri katika maisha yetu”, alisema.

Pamoja na mambo mengine, Askofu huyo alifafanua kuwa hivi sasa kuna kila sababu kwa Wilaya zilizopo mkoani Ruvuma kwa ujumla, zitenge chakula cha kutosha katika maeneo yao kwa kuhamasisha wananchi wazalishe chakula kwa wingi ili njaa isiweze kutokea na kutesa jamii.

Hata hivyo akielezea suala la upungufu wa madawati katika shule za msingi na sekondari ambalo linaendelea kutesa wanafunzi mashuleni hapa nchini, alisema kuwa viongozi katika maeneo yao wanapaswa kulitekeleza kwa wakati uliopangwa ili wanafunzi darasani waweze kuondokana na adha ya wanayoipata sasa, ya kukaa chini na kushindwa kuzingatia vizuri vipindi vya masomo wanapokuwa darasani.








No comments: