Friday, February 26, 2016

HALMASHAURI MJI WA MBINGA YAAZIMIA KUNUNUA MTAMBO WA KUSAGA TAKA




Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALMASHAURI ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, imeazimia kununua mitambo maalum ya kusaga takataka, ili kuondokana na hatari ya kukumbwa na magonjwa ya milipuko yanayotokana na uchafu ikiwemo kipindupindu.

Akizungumza katika kikao cha baraza la Madiwani, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Oscar Yapesa alisema kuwa takataka hizo pia zitakuwa zikisagwa kwenye mitambo hiyo, na kutumika kama mbolea kwenye mashamba ya wakulima.
Oscar Yapesa.

Kadhalika Mkurugenzi huyo alisema kwamba, wanakabiliwa na changamoto ya gari la kuzoa taka hizo ambapo hivi sasa wanagari moja tu ambalo halitoshelezi mahitaji halisi.

Naye Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga kwa upande wake aliwataka Madiwani hao kuhakikisha wanawaelimisha wananchi ya juu ya utunzaji wa mazingira, ili kuepukana na ugonjwa huo wa kipindupindu.

Kwa ujumla Halmashauri ya mji wa Mbinga, inazalisha takataka tani 18 kwa siku na ina uwezo wa kuzoa tani tatu tu kwa siku jambo ambalo linatishia afya za wakazi wa mji huo, wakihofia kukumbwa na magonjwa ya mlipuko yanayotokana na uchafu.

No comments: