Thursday, February 18, 2016

WAFANYABIASHARA WANAOUZA MITUMBA SONGEA WALIA NA SERIKALI



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WAFANYABIASHARA wanaouza nguo za mitumba na bidhaa nyingine katika eneo maarufu la majengo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamelalamikia  kitendo cha eneo hilo kuwa na tope linalosambaa barabarani hadi  kwenye vibanda  vyao vya biashara, na kusababisha kero kubwa kwao na wateja wao.

Walisema kuwa hali hiyo inatokana na barabara inayopita katikati ya eneo hilo kutofanyiwa  matengenezo kwa muda mrefu, baada ya Manispaa hiyo kuondoa tabaka la lami lililokuwa  hapo awali kwa madai ya kuweka lami  mpya, hata hivyo ni muda wa miaka mitano sasa umepita hakuna matengenezo mapya yaliyofanyika tangu tabaka hilo la lami litolewe.

Walisema wamekuwa wakifanya shughuli zao katika  mazingira magumu na mateso makubwa, hasa kipindi hiki cha masika na kwamba wakati wa kiangazi kunakuwa na vumbi ambalo husambaa na kuchangia kuharibika kwa bidhaa zao wanazoziuza.


Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao, hali hiyo imepelekea kuwa na maisha magumu na hata idadi ya wateja wao inazidi kupungua huku baadhi yao kutopenda tena kwenda kununua bidhaa zao, wakihofia usalama wa bidhaa wanazozinunua na magari yao kutokana na kuwepo mashimo makubwa katika barabara hiyo, yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha sasa.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake mmoja wa wafanyabiashara aliyejitambyulisha kwa jina la,  Abdallah Said (34) alisema kero nyingine kubwa wanayokumbana nayo katika msimu huu wa mvua, baadhi ya maeneo yanajaa maji na kusababisha  barabara hiyo kuchimbika na kwamba hata akina mama wanaojishughulisha kuuza matunda na mbogamboga huwawia vigumu kufanya biashara zao kutokana na mazingira kuwa mabaya.

Kadhalika Said aliiomba serikali kuchukua hatua za haraka kuifanyia matengenezo barabara hiyo, kwani imekaa kwa muda wa miaka mingi bila kufanyiwa matengenezo na kwamba barabara hiyo inayolalamikiwa ni ile inayoanzia hotel maarufu ya Swiss kuelekea mtaa wa Majengo magengeni ambayo inapita katikati ya eneo  la wafanyabiashara hao wa mitumba, ikielekea kata jirani ya Ruvuma katika Manispaa hiyo ya Songea.

No comments: