Wednesday, February 24, 2016

MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA KONDOA HUSSEIN NGAGA AKALIA KUTI KAVU

Hussein Issa Ngaga, Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma.


Na Dany Tibason,
Dodoma.

SELEMAN JAFO, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) amebaini upotevu wa shilingi milioni 180 katika Halmashauri ya wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma.

Kutokana na kubainika kwa upotevu wa fedha hizo, Jafo ametoa masaa 48 kwa Hussein Issa Ngaga ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, ahakikishe anapeleka maelezo ya kina katika Ofisi ya TAMISEMI juu ya kuibiwa kwa fedha hizo ambazo ni za walipakodi Watanzania.

Agizo hilo la Naibu Waziri huyo, lilitokana na ziara yake ya kikazi aliyoifanywa jana sambamba na kufanyika kwa kikao cha ndani, katika Halmashauri hiyo.

Alisema kuwa, serikali ya awamu ya tano haitavumilia kiongozi yeyote ambaye atafanya ubadhirifu wa fedha za umma au jambo lolote ambalo linaonekana kuwepo na harufu ya ufisadi.


Jafo alifafanua kuwa nchi imekuwa ikiendeshwa kimazoea na watu kujilimbikizia mali, bila kuwa na hofu ya kuhojiwa jambo ambalo linawafanya watumishi wa umma kuwa na kiburi na kufanya kile wanachofikiria.

“Nchi imekuwa ikiendeshwa kimazoea sana, watu wanakula hela bila utaratibu na wanafunika funika tu mambo huku wakiwafanya watu kama vipofu, hili halitavumiliwa hata kidogo, lazima hatua stahiki zichukuliwe,” alisema.

Alibainisha kuwa anataka maelezo ya kina juu ya wizi wa fedha hizo na ndani ya masaa hayo 48, awe amepata taarifa kamili pale ofisini kwake.

Sambamba na hilo, aliagiza watu nane wanaotuhumiwa kuhusika na wizi wa fedha hizo, wasimamishwe kazi na kukaa pembeni kupisha uchunguzi.

Aidha amewaagiza maofisa utumishi na wakuu wa idara, kuwajibika na kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kuachana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.

Naibu wiziri huyo ameeleza kuwa kumekuwepo na malalamiko mengi juu ya watendaji wake ngazi ya chini, ambao wamekuwa wakionewa na kutopatiwa haki zao kama inavyostahili.

Alisema, watumishi hao wanalalamika kutolipwa malimbikizo yao mbalimbali kama fedha za likizo na kutopandishwa vyeo kwa wakati.

No comments: