Saturday, February 13, 2016

JIPU LATUMBULIWA SONGEA MHANDISI WA UJENZI ASIMAMISHWA KAZI



Na Kassian Nyandindi,

Songea.

HALMASHAURI ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kupitia baraza lake la Madiwani wa Halmashauri hiyo limemsimamisha kazi Mhandisi wa idara ya ujenzi Daud Basilio, kwa sababu ya uzembe wa kutokuwa kazini kwa muda mrefu, ubadhirifu wa fedha na kutokuwa makini katika kusimamia miradi mbalimbali ya idara hiyo.

Akitoa taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Rajabu Mtiula alisema, pia wamechukua hatua hiyo baada ya mhandisi huyo, kuisababishia halmashauri hasara ya shilingi milioni 38,186,400.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Mtiula alisema kuwa katika kikao chake cha dharula kilichoketi juzi mjini hapa, kimeamua kumweka pembeni mhandisi Basilio kutokana na licha ya kuonywa mara kwa mara na baraza hilo la madiwani, amekuwa akipuuza na kushindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo, ikiwemo kushindwa kusimamia kikamilifu miradi mbalimbali ya wananchi inayotekelezwa katika idara ya ujenzi.

Alifafanua kuwa mhandisi huyo, amekuwa akitumia taaluma yake vibaya ambapo amekuwa akishirikiana na wakandarasi kuihujumu halmashauri na kuisababishia hasara kubwa ya fedha, kitendo ambacho kinawakosesha wananchi kupata huduma stahiki.


Mwenyekiti huyo wa halmashauri ya wilaya ya Songea alieleza kuwa, pia ameshindwa kusimamia ujenzi wa barabara ya kutoka Mpitimbi kwenda Mbinga Mhalule na kuidhinisha mkandarasi husika alipwe shilingi milioni 27,082,500 jambo ambalo linadhihirisha wazi kuwa ni ubadhirifu wa fedha za umma.

Kadhalika aliongeza kuwa Basilio amehujumu ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao ya chakula katika kata ya Mgazini kwa kumlipa mkandarasi aliyejenga ghala hilo shilingi milioni 11,103,900 kinyume na taratibu, kabla ujenzi wake haujakamilika kwa viwango vinavyokubalika.

Mtiula alisema kwamba, kufuatia hali hiyo madiwani baada ya kuchaguliwa na kuapishwa walitembelea miradi hiyo huku wakiwa wameambatana na wataalamu wa halmashauri yake na kuweza kubaini matatizo hayo, yaliyopo katika miradi hiyo.

Alisema waliweza kubaini mapungufu mengi, ambayo waliona ni vyema mhandisi huyo akae pembeni huku taratibu zingine za kumwajibisha zikiendelea kuchukuliwa na kufuata mkondo wake, kama vile taratibu za utumishi wa umma zinavyotaka.

Pamoja na mambo mengine, madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Songea wamemtaka Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Sixbert Kaijage kuwasimamia kikamilifu wataalamu wake ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi na uadilifu mkubwa, ili matatizo kama hayo yasiweze kutokea tena.

Kwa upande wake akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi huyo mtendaji wa wilaya hiyo alisema amesikitishwa na kitendo alichokifanya mhandisi huyo cha kutumia taaluma yake vibaya, kwa kumshauri kuidhinisha malipo hewa yenye harufu ya rushwa na ubadhirifu.

Kaijage aliwataka watumishi wote wa halmashauri yake kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu husika, ili kuweza kuleta maendeleo kwa wananchi kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

Awali katika kikao hicho cha baraza la madiwani halmashauri ya wilaya ya Songea ambacho kiliketi hivi karibuni, kilimsimamisha kazi Kaimu Mhandisi wa idara ya maji wa wilaya hiyo, John Undili kwa sababu ya uzembe na kutokuwa makini katika kusimamia miradi mbalimbali ya maji na kuisababishia halmashauri hiyo, hasara ya mamilioni ya fedha.

No comments: