Monday, February 15, 2016

SERIKALI KUPELEKA MADAKTARI BINGWA MAENEO YA PEMBEZONI IKIWEMO MKOA WA RUVUMA

 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Dkt. Hamis Kigwangalla akiangalia moja ya vitanda vinavyotumika katika upasuaji Hospitali ya mkoa wa Ruvuma, ambapo aliambiwa changamoto kubwa baadhi ya taa za vitanda hivyo kuwa na hitilafu.


Na Mwandishi wetu,
Songea.

NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Dkt. Hamis Kigwangalla amesema wizara yake itahakikisha inapeleka Madaktari bingwa katika mikoa mbalimbali hapa nchini, ikiwemo hospitali ya mkoa wa Ruvuma, ili kuweza kuleta ufanisi mzuri wa utendaji kazi katika sekta hiyo ya afya.

Hayo yalisemwa na Dkt. Kigwangalla wakati alipokuwa katika ziara yake mkoani humo, aliyoifanya mapema hivi karibuni Februari 13 mwaka huu.


Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Naibu Waziri huyo mjini Songea, baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma na kituo cha afya Mjimwema, kilichopo mjini hapa.

Dkt. Kigwangalla aliitaka mikoa ya pembezoni ukiwemo mkoa huo, kujiandaa na kuweka mazingira mazuri ya kuwavutia madaktari bingwa, ili waweze kufanya kazi zao ipasavyo pindi serikali itakapowaleta.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu alisema kuwa mkoa huo umeridhishwa na staili ya ziara ya kushtukiza na kwamba wanajitahidi kuboresha vituo vya afya vya Mjimwema Songea, Madaba na cha wilaya ya Namtumbo ili vipandishwe hadhi kuwa hospitali za wilaya.

Kadhalika Dkt. Kigwangalla alipata wasaha wa kutembelea maeneo mbalimbali na kujionea utendaji wa kazi, huku akitoa msisitizo katika suala la maboresho zaidi.

No comments: