Friday, February 12, 2016

MKUU WA WILAYA MBINGA AWATAKA VIONGOZI KUACHA TABIA YA KUJIKWEZA NA KUWA MIUNGU WATU



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

SENYI Ngaga ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, amewataka viongozi wa wilaya hiyo kuacha tabia ya kujikweza na kuwa miungu watu badala yake wajenge ushirikiano na wananchi katika kutatua kero mbalimbali kwa wakati, ili waweze kuendana na kasi ya utendaji kazi wa serikali hii ya awamu ya tano.

Ngaga alisema kuwa ni jukumu la kila kiongozi wilayani humo kujituma kikamilifu katika utekelezaji majukumu ya wananchi, huku akisisitiza suala la ukusanyaji wa mapato kikamilifu na kuzuia mianya ya upotevu wa mapato hayo.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga.

“Mkurugenzi na wataalamu wako, nawaagiza simamieni kikamilifu kipengele hiki cha ukusanyaji mapato kwa kutumia mifumo ya kisasa ambayo serikali imeagiza, pia kuweni  wabunifu wa vyanzo vipya vya mapato ili kuweza kuongeza kiasi cha fedha ambazo zitaweza kuhudumia jamii katika shughuli mbalimbali za maendeleo”, alisisitiza Ngaga.

Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga, alitoa rai hiyo juzi alipokuwa akitoa salamu za serikali katika kikao cha kawaida cha baraza la madiwani la wilaya hiyo, kilichoketi kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.


Akizungumzia suala la elimu aliwataka wadau wa sekta hiyo muhimu kuhakikisha kwamba, kupitia vikao vyao vya kamati za shule waelimishe wazazi kuchangia chakula kwa shule za msingi na sekondari za kutwa ili watoto wanaosoma katika shule hizo, waweze kupata chakula na kuwafanya kuhudhuria vipindi vya masomo darasani kikamilifu.

Ngaga alifafanua kuwa ni jukumu la kila mmoja wetu kusimamia suala la elimu na kwamba, serikali haijafuta suala la uchangiaji chakula mashuleni hivyo mzazi ni lazima achangie, ili kuondokana na kero ya mtoto kukaa na njaa wakati anapokuwa shuleni.

“Utaratibu wa mzazi kuchangia upo pale pale, tukae na kuzungumza na wazazi wetu tuwaelimishe juu ya taratibu zipi wanatakiwa kuzifuata na kutekeleza, kwa yale yaliyoagizwa na serikali tuyaweke wazi ili siku ya mwisho tukiwa na uelewa wa pamoja, tuweze kufikia malengo husika”, alisema Ngaga.

Vilevile alipongeza jitihada zinazofanywa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Venance Mwamengo juu ya utengenezaji wa madawati kwa shule za msingi na sekondari wilayani humo, ambazo zina upungufu wa madawati ya kukalia wanafunzi.

Hata hivyo Ngaga alibainisha kwamba Mkurugenzi huyo, kwa kasi aliyonayo ya utekelezaji wa suala hilo anahakika tatizo la upungufu wa madawati 12,600 lililopo katika wilaya yake, litakwisha mapema na kuwafanya wanafunzi katika shule hizo waweze kuondokana na kero hiyo ambayo imedumu kwa muda mrefu sasa.

No comments: