Saturday, February 13, 2016

MIEZI SITA JELA KWA KUMILIKI SILAHA KINYUME NA TARATIBU ZA NCHI



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI mmoja anayeishi mtaa wa Misufini Tunduru mjini hapa mkoani Ruvuma, Mohamed Rashid Linyama (42) amehukumiwa kutumikia kifungo cha miezi sita jela baada ya kupatikana kosa la kukutwa na silaha kinyume cha  sheria na taratibu za nchi, juu ya umiliki halali wa silaha na risasi zake.

Adhabu hiyo imetolewa na Mahakama ya wilaya ya Tunduru, na kutoa amri ya kutaifishwa kwa bunduki hiyo na kuwa mali ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hakimu wa  Mahakama ya wilaya hiyo, Gladys Barthy alitoa hukumu hiyo baada ya mtuhumiwa kukiri kufanya kosa hilo na kuifanya Mahakama kumtia hatiani kwa kosa lililokuwa likimkabili.

Awali akisoma shikata hilo lenye jinai namba 4/2016 mwendesha mashtaka  wa Mahakama hiyo, mkaguzi msaidizi wa Polisi Inspekta Songelael Jwagu alisema kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Disemba 31 mwaka jana, akiwa na  bunduki katika kijiji cha Likweso majira ya asubuhi.

Katika hati ya mashtaka hayo mtuhumiwa  Linyama pia alikuwa na shitaka namba 2/2016 lililokuwa likimkabili juu ya wizi wa pikipiki aina ya Sunlg, yenye namba za usajili MC 670 ACG aliyokutwa akiwa anaitumia siku alipokamatwa na bunduki hiyo, kosa ambalo nalo liliondolewa baada ya mmliki wa pikipiki hiyo, kujitokeza na kukabidhiwa.


Alisema katika tukio hilo, Linyama alikutwa akiwa na bunduki aina ya Maka Four (IV) yenye namba za usajili F 8646 akimiliki kinyume na taratibu za nchi.

Inspekta Jwagu aliendelea kufafanua kuwa  kitendo hicho cha kumiliki silaha bila kufuata taratibu husika, ni kosa na kinyume cha sheria namba 4 (1) cha kanuni ya adhabu sura ya 223 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
 
Baada ya mtuhumiwa huyo kutiwa hatiani na Mahakama hiyo, mwendesha mashtaka huyo wa Polisi aliiomba Mahakama kumpatia adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine, ambao wamekuwa na tabia kama hiyo.

Akitoa utetezi wake mbele ya Mahakama hiyo, mtuhumiwa huyo aliiomba Mahakama kumpatia adhabu ndogo kwa vile anaishi na watoto watano, mke na wazazi wake ambao wanamtegemea na baadaye Mahakama ilimhukumu adhabu ya kwenda miezi sita jela.

No comments: