Sunday, February 7, 2016

ATIWA MBARONI KWA KUFANYA MAPENZI NA WANAFUNZI WATATU



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, limemtia mbaroni Kassim Millinga (52) ambaye ni mkazi wa Lizaboni Manispaa ya Songea mkoani humo, kwa tuhuma za kuwabaka wanafunzi watatu wanaosoma darasa la sita shule ya msingi ya Kibulang`oma iliyopo mjini hapa.

Akizungumza na gazeti hili Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zuberi Mwombeji alisema kuwa tukio hilo limetokea kwa nyakati tofauti katika eneo la Lizaboni jirani na shule hiyo wanayosoma wanafunzi hao, ambao wote wana umri wa miaka 12 kila mmoja na majina yao yamehifadhiwa.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji.
Kamanda huyo wa Polisi alisema kuwa Millinga ambaye pia anafanya kazi ya ulinzi kwenye kampuni ya ulinzi ya Ilonjezi iliyopo mjini Songea, anatuhumiwa kwamba kwa nyakati tofauti tangu mwaka jana amekuwa akiwarubuni wanafunzi hao kwa kuwapa pesa, chakula na nguo kisha kuwalazimisha kufanya nao mapenzi kwenye nyumba anayoishi huku akiwatishia kutosema kwa mtu yeyote kuhusiana na kitendo hicho anachowafanyia.


Alifafanua kwamba Januari 26 mwaka huu, majira ya saa nane mchana wanafunzi hao wakiwa kwenye eneo la shule wanayosoma walikutwa na mwalimu mmoja (Jina limehifadhiwa) wa shule hiyo, wakiwa wanagombania shilingi 1,500 ambazo inadaiwa walikuwa wamepewa na Millinga na kwamba alipowaona wanaendelea kugombana juu ya fedha hizo, alilazimika kuingilia kati ili aweze kujua chanzo chake ni nini.

Alieleza zaidi kuwa, baada ya kuwauliza ni sababu gani inawafanya wagombee fedha hizo huku akiwabana wamueleze wamezipata wapi ndipo wanafunzi hao walimjuza Mwalimu wao jinsi walivyofanyiwa na Milinga na kwamba, fedha hizo alikuwa amewapa baada ya mmoja wao kufanya naye mapenzi.

Kamanda Mwombeji alifafanua kuwa wanafunzi hao walimweleza mwalimu wao kuwa tangu mwaka jana, wamekuwa wakifanya mapenzi na Millinga kwa nyakati tofauti ambapo amekuwa akiwapa vitu mbalimbali ikiwemo pesa, nguo, na chakula jambo ambalo mwalimu huyo lilimshitua na kumlazimu kutoa taarifa kwa uongozi wa shule kisha taarifa hizo kufikishwa kwenye kituo kikuu cha Polisi Songea mjini.

Alisema kuwa Polisi baada ya kupata taarifa ya tukio hilo, walimsaka mtuhumiwa Millinga na baadaye walifanikiwa kumkamata ambapo katika mahojiano ya awali alikiri kufanya mapenzi na wanafunzi hao, huku akieleza kuwa walikuwa wanaenda kufanya kazi ya kumpigia deki chumbani kwake katika nyumba anayoishi mtaa Lizaboni mjini hapa.

Pamoja na mambo mengine, Kamanda huyo wa Polisi mkoani Ruvuma alisema kuwa uchunguzi bado unaendelea kuhusiana na tukio hilo na muda wowote kuanzia sasa utakapokamilika, mtuhumiwa huyo atafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili.

No comments: