Wednesday, February 17, 2016

HUDUMA MPYA YA KITABIBU INAYOMWEZESHA MGONJWA KUFANYIWA UPASUAJI KWA NJIA YA VITUNDU KUTOLEWA HOSPITALI YA RUFAA MBEYA

Wataalamu ambao ni madaktari wa upasuaji, wakiwa katika chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Rufaa Jijini Mbeya.
Na Mwandishi Maalum,

Mbeya.

HUDUMA mpya ya kitabibu imeanza kutolewa katika Hospitali ya rufaa ya Kanda Jijini Mbeya, itakayomwezesha mgonjwa kufanyiwa upasuaji kwa njia ya vitundu (Laparoscopic Surgery) na hivyo kumwezesha kupona mapema na kuwahudumia wagonjwa wengi kwa muda mfupi. 

Huduma hiyo ya upasuaji, ambayo hutumia mashine inayofahamika kwa jina la Mnara wa Upasuaji wa Vitundu au kwa lugha ya kizungu, Laparoscopic Tower inalenga kutumia muda mfupi wa upasuaji na kumuwezesha mgonjwa kupata naafuu mapema.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi daktari bingwa wa upasuaji katika hospitali hiyo ya Rufaa, Dkt. Lazaro Mboma alisema kuwa mashine hiyo itamwezesha mgonjwa kurudi katika shughuli zake za kawaida muda mfupi, baada ya upasuaji kutokana na kutokuwa na kidonda kikubwa badala yake mgonjwa atakuwa akiuguza vidonda vidogo vya matundu, yaliyotumika wakati wa upasuaji.


Pamoja na hayo alisema pia kwa siku ya kwanza yaani leo, wagonjwa wawili waliokuwa na matatizo ya mawe katika mfuko wa nyongo wamefanyiwa upasuaji wa mafanikio ambapo kazi hiyo, imekwenda sambamba na kuwapa mafunzo madaktari wengine wa hospitali hiyo juu ya matumizi ya mashine hiyo.  

Aidha Dkt. Mboma alisema mashine hiyo inawahusu wagonjwa wote, wale wanaotumia bima za afya na wasionazo lakini kutokana na gharama za uendeshaji inawalazimu madaktari kuwahudumia kwanza wagonjwa wanaohudumiwa kwa bima ya afya, hivyo amewashauri wananchi kujiunga na mfuko huo wa bima ya afya kwani kwa mgonjwa wa kawaida ni ngumu kumudu gharama zake za matibabu. 

Madaktari waliofika Jijini Mbeya kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa madaktari wa hospitali hiyo ni Profesa Hening na mtaalamu wa mashine hiyo, Frolian Bets ambao wataendelea kuwepo Mbeya kwa siku tatu ili kuwawezesha madaktari wa hospitali hiyo ya Rufaa, kupata ujuzi wa kutumia mashine hiyo. 

Naye mkuu wa idara ya upasuaji katika hospitali hiyo ya Rufaa, Dkt. Mujuni Mutagwaba alitoa wito kwa wakazi wa Mbeya na mikoa ya Nyanda za juu kusini kujitokeza kwa wingi, kwenda kutibiwa katika hospitali hiyo ili kuokoa maisha yao na kupata tiba stahiki. 

Mashine ya kitabibu ya Mnara wa Upasuaji wa Vitundu (Laparoscopic Tower) ni ya kwanza mkoani Mbeya na kwamba vipo vituo vichache Tanzania, vilivyo na mashine ya upasuaji ya aina hiyo hivyo husababisha wagonjwa wengine kusafiri kwenda nchi za nje, kwa ajili ya kupata tiba kwa njia hiyo.

No comments: