Thursday, February 18, 2016

MWAMBUNGU ATOA MIEZI SITA KWA WAKURUGENZI RUVUMA KUMALIZA TATIZO LA MADAWATI



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu ametoa miezi sita kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Wilaya na Manispaa mkoani humo, wahakikishe kwamba wanamaliza tatizo la ukosefu wa madawati katika shule zote za msingi na sekondari ambazo zinamilikiwa na serikali, na kwamba Mkurugenzi atakayeshindwa kutekeleza agizo hilo hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu huyo wa mkoa, alipokuwa akizungumza na Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani humo kwenye kikao maalum cha bajeti na mpango wa maendeleo ya wilaya hiyo, kilichoketi mjini hapa.

Said Thabit Mwambungu.
Mwambungu alisema kuwa kila halmashauri zinapaswa kutumia rasilimali zake ikiwemo misitu, kwa ajili ya kutengenezea madawati huku akiongeza kuwa hakuna sababu ya wanafunzi kukaa chini wakati mkoa huo, una miti mingi ya mbao.

Aidha Mwambungu amewataka Madiwani katika mkoa huo, kujenga ushirikiano na serikali kwa kuwafichua wazazi wasiopeleka watoto wao shule ili wachukuliwe hatua za kisheria.


Vilevile amewataka walimu kuacha tabia ya kuwarudisha nyumbani, wanafunzi ambao wazazi wao wameshindwa kulipa michango ya chakula na kwa yule atakayebainika kufanya hivyo, sheria itachukua mkondo wake ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Kadhalika amewataka Wakurugenzi hao kukamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara kwa shule za sekondari, ili watoto viweze kuwasaidia wakati wanaposoma masomo ya sayansi kwa vitendo.

Pamoja na mambo mengine kikao hicho cha baraza la Madaiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Songea, kimepitisha bajeti na mpango wa maendeleo yake kwa mwaka 2016/2017 kiasi cha shilingi bilioni 34,881,982,411 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo, huku kipaumbele wakizingatia kuboresha sekta ya elimu, afya na maji.

No comments: