Thursday, February 18, 2016

WATENDAJI HALMASHAURI WILAYA YA NYASA WATAKIWA KUONGEZA UFANISI KATIKA MAENEO YAO YA KAZI




Na Mwandishi wetu,
Nyasa.

MKURUGENZI mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Jabir Shekimweri amewataka watumishi wa halmashauri hiyo, kuongeza ufanisi wa utendaji katika maeneo yao ya kazi ili kwa pamoja waweze kutekeleza na kufanikisha kwa vitendo, mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN).

Shekimweri ametoa agizo hilo jana, alipokuwa akizungumza na watendaji wa vijiji, mitaa, kata katika kikao maalumu cha kazi wilayani humo ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya serikali kwa kuwataka viongozi  na wakuu wa idara zake, kuwa na vikao vya mara  kwa mara na watumishi waliochini yao ikiwa ni lengo la kupata majawabu na kero zinazowakabili wananchi.

Ziwa Nyasa.
Alisema kuwa watendaji hao wanawajibu mkubwa katika kufanikisha mpango huo wa BRN, kwa kusimamia vizuri miradi na fedha zinazoelekezwa kwenye maeneo  yao kama ilivyoagizwa na serikali.

“Tunataka kuona katika kipindi cha mwaka mmoja na kuendelea kuna kuwepo na mabadiliko makubwa hususan kwenye miradi ya maendeleo, ambayo imeainishwa kwenye mpango wa matokeo makubwa sasa”, alisema Shekimweri.

Vilevile alifafanua kuwa katika utekelezaji wa mpango huo, halmashauri yake  imejipanga kuhakikisha kwamba inafanya vyema katika usimamizi na hata utekelezaji wake, ili iweze kuleta tija kama ilivyokusudiwa.


Aidha alisisitiza kwamba hatowafumbia macho watumishi wazembe, ambao kwa namna moja au nyingine watabainika kukwamisha kwa makusudi utekelezaji  wake, ambapo ameonya kwa kuwataka watumishi waache kufanya kazi kwa mazoea kwani hivi sasa ataanza kuangalia upya juu ya utendaji wao wa kazi za kila siku.

Pia alisema hatakubali kuona  kuna kundi kubwa la watumishi ambao ni mizigo kazini ambao hawawajibiki ipasavyo kwa wananchi, jambo ambalo litakuwa ni tatizo katika ufanisi wa mpango huo na kukwamisha maendeleo kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

No comments: