Thursday, February 11, 2016

MADIWANI MBINGA WAPITISHA BAJETI SHILINGI BILIONI 49.4 KWA AJILI YA UTEKELEZAJI MAENDELEO YA WANANCHI KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga vijijini mkoani Ruvuma, Venance Mwamengo (upande wa kulia) akisisitiza jambo katika kikao cha baraza la madiwani la wilaya hiyo. Katikati ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ambrose Nchimbi na Makamu wake Bernad Komba. 


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, katika rasimu yake ya bajeti ya mwaka 2016/2017 imekisia kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi bilioni 49.4 kwa ajili ya utekelezaji na kuboresha shughuli mbalimbali, za maendeleo ya wananchi wilayani humo.

Katika fedha hizo shilingi bilioni 32.5 zinalenga kulipa mishahara ya wafanyakazi wake, bilioni 3.9 matumizi mengine, bilioni 9.0 ni fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Aidha imekisia kukusanya na kutumia shilingi bilioni 3.8 ambazo ni fedha zitakazotokana na makusanyo ya ndani, katika halmashauri ya wilaya hiyo. 


Hayo yalisemwa na Ofisa mipango wa wilaya hiyo, Onesmo Mapunda wakati alipokuwa akiwasilisha umbile la makisio hayo ya matumizi ya fedha katika rasimu ya bajeti ya wilaya hiyo, kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017.

Mapunda alikuwa akiwasilisha kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Venance Mwamengo kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichoketi Februari 10 mwaka huu, ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.

Pia alisema kuwa fedha hizo zitajikita hasa katika kuboresha huduma kwenye sekta ya elimu, afya, maji, kilimo na mazingira ili kuweza kutoa huduma endelevu za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wake.

Alibainisha kuwa wananchi hao wataweza pia kuwapunguzia kero wanazokabiliana nazo, hivyo kusaidia juhudi ya kupunguza umaskini na kuboresha maisha yao kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

Pamoja na mambo mengine, Ofisa mipango wa wilaya ya Mbinga Mapunda aliongeza kwamba, bajeti iliyopita ya mwaka 2015/2016 fedha ambazo waliidhinishiwa na serikali kwa ajili ya matumizi mbalimbali wameweza kufikia malengo mazuri ya utekelezaji wa miradi ya wananchi na kuifanya wilaya, iweze kusonga mbele kimaendeleo.

No comments: