Friday, February 5, 2016

WALIOBOMOLEWA NYUMBA TUNDURU KUPISHA UJENZI WA BARABARA KULIPWA FIDIA ZAO

Rais mstaafu Dokta Jakaya Mrisho Kikwete (katikati) na aliyekuwa balozi mdogo wa Japan hapa nchini Kazuyoshi Matsunaga (wa tatu kushoto) wakishirikiana kukata utepe ikiwa ni ishara ya kuzindua ujenzi wa barabara ya Tunduru-Mangaka Matemanga mradi unajengwa na Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wa serikali ya Japan kupitia shirika lake la kimataifa la maendeleo JICA. Tukio hilo lilifanyika mwaka 2014.

Na Steven Augustino,
Tunduru.

IMEELEZWA kuwa wahanga 280 ambao walibomolewa nyumba zao, kwa lengo la kupisha ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami katika vijiji vilivyopo kwenye tarafa ya Nakapanya wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, hivi sasa wameweza kutimiza vigezo vya kuishawishi serikali kulipwa fidia zao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyoufikia mtandao huu, imefafanuliwa kuwa wahanga hao ni kati ya wananchi 352 ambao walipeleka malalamiko yao, ya kuomba kuongezewa fidia kwa madai kwamba awali hawakuridhishwa na malipo ya fidia waliyolipwa awamu ya kwanza.

Taarifa hiyo ilitolewa na mwakilishi wa dawati la kusikiliza migogoro kutoka makao makuu ya Wakala wa barabara hapa nchini (TANROADS), Gibson Mwaya wakati alipokuwa akitoa taarifa kwa wahanga hao, waliokuwa wamekusanyika katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo, kwa ajili ya kufuatilia hatima ya   madai yao.


Akifafanua taarifa hiyo, Mwaya alisema  kwamba wahanga 72 kati ya 352 wameshindwa kutimiza vigezo vya kulipwa fidia kutokana na kushindwa kutimiza matakwa husika na akawashauri wajipange upya na kupeleka malalamiko yao kupitia wataalamu, ambao watawatembelea katika maeneo yao vijijini kwa lengo la kusikiliza kero zao.

Mwaya alibainisha kuwa  wahanga hao ni wale wa kutoka vijiji  vya Songambele, Namakambale, Nakapanya, Pacha ya mindu, Mtonya, Misufini, Namiungo, Mnazi mmoja na Majimaji wilayani Tunduru.

Alisema kuwa kwa upande wa wananchi waliobomolewa nyumba zao kuanzia vijiji vya Muhuwesi, Chingulungulu, Msagula, Sevuyanke, Temeke, Sisi kwa sisi, Mkapunda, Ngalinje, Mchangani, Kalonga, Lambai na Tunduru mjini ambao hawajalipwa kabisa wajiandae kukutana na kamati  itakayopita kufanya tathimini kuanzia mwezi Februari mwaka huu.

Hata hivyo alisema katika zoezi hilo, timu hiyo itachukua kero na malalamiko mbalimbali kutoka kwa wahanga hao na amewataka wajiandae na vielelezo vya madai yao, ili kupunguza muda wa kuwasikiliza na kufanya kazi hiyo iweze kukamilika kwa wakati.

No comments: