Monday, February 22, 2016

JELA MIEZI 12 KWA KUKUTWA NA NYARA ZA SERIKALI



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI mmoja wa kijiji cha Chiungo wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, Rashid Selemani (41) amehukumiwa kwenda jela kutumikia kifungo cha miezi 12, baada ya kupatikana na hatia katika makosa matatu yaliyokuwa yakimkabili.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Tunduru, Gradys Barthy baada ya Mahakama hiyo, kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Awali akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu huyo, Mwendesha mashtaka mkaguzi msaidizi wa Polisi Inspekta Songelaele Jwagu alisema mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa anakabiliwa na makosa matatu, kosa la kwanza  bila halali alipatikana na nyara za serikali, kinyume na kifungu namba 86 (1) na kifungu cha 2 (b) cha sheria ya kuhifadhi wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009. 

Akifafanua maelezo ya kosa hilo, alisema mnamo Juni 27 mwaka jana majira ya mchana katika hifadhi ya Mwambesi wilayani Tunduru mkoani hapa, mshitakiwa huyo alikamatwa akiwa na nyama ya ngorombwe, ngozi na nyama ya sungura bila kibali.


Kwa mujibu wa hati ya mashtaka hayo, kosa la pili lililokuwa likimkabili mtuhumiwa huyo ni kupatikana na mitego ya kuwindia wanyama bila kibali kinyume na kifungu namba 65 (1) (a) (ii) na 5 cha sheria ya uhifadhi wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009.

Akifafanua maelezo ya kosa hilo, Inspekta Jwagu alisema kuwa mnamo Juni 27 mwaka jana majira hayo ya mchana katika hifadhi ya Mwambesi wilayani humo, alikamatwa akiwa na mitego 20 ya kuwindia wanyama hao.

Kosa la tatu lililokuwa likimkabili mtuhumiwa huyo, pia kuingia katika hifadhi ya Taifa bila kibali kinyume na kifungu namba 15 (1) na 2 cha sheria ya kuhifadhi wanyama pori na sheria namba 5 ya mwaka 2009.

Katika kuthibitisha makosa hayo, upande wa mashtaka ulileta mashahidi wake wanne kwa lengo la kuithibitishia Mahakama hiyo, na baadaye sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Baada ya kumtia hatiani alitakiwa kulipa faini ya shilingi  900,000 kwa kosa la kwanza na la pili  100,000 huku la tatu 50,000 au kwenda jela miezi 12 endapo atashindwa kulipa faini.

Katika utetezi wake mtuhumiwa huyo, aliiomba Mahakama hiyo kumpunguzia adhabu hiyo kwa sababu ana watoto watano, mke na anategemewa na mama yake mzazi ambaye sasa ni kikongwe hata hivyo Mahakama, ilitupilia mbali ombi lake na alishindwa kulipa faini hizo ambapo aliishia kwenda jela.

No comments: